Dawa ya wadanganyifu mitihani ni kuwajibishwa

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 08:18 AM Jan 07 2025
 Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed
Picha:Mtandao
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA), limefuta matokeo yote ya wanafunzi 105 wa darasa la nne na 46 wa kidato cha pili kwa maelezo ya kufanya udanganyifu na kuandika matusi.

Mbali na hatua hiyo, NECTA pia imekifungia kituo cha Upimaji na Mitihani ya Taifa GoodWill cha Arusha kutokana na mkuu wa shule na baadhi ya walimu kuthibitika kufanya udanganyifu ili kusaidia wanafunzi.
 
 Ni kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed, akitangaza matokeo hayo wiki iliyopita, akifafanua kuwa yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5(2)(j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani  pamoja na kifungu cha 30(2) (b) cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016.
 
 Katika ufafanuzi wake wanafunzi hao 100 wa darasa la nne walifanya udanganyifu na watano waliandika matusi huku kwa kidato cha pili waliofanya udanganyifu ni 41 na watano waliandika matusi katika karatasi zao za majibu katika upimaji wa kitaifa wa kidato hicho.
 
 Inaelezwa na Katibu Mkuu kuwa kati ya wanafunzi hao 100 waliofutiwa matokeo, 98 walipangwa na walimu wakuu kuwafanyia wanafunzi wenzao mitihani kwa maslahi binafsi.
 
 Nikirejea kwenye hoja yangu ni kwamba, kwa kuwa udanganyifu umekuwa wa miaka nenda miaka rudi, baraza lingeanzia kwa walimu hao kubaini mianya yote ya udanganyifu na kuidhibiti.
 
 Walimu waliobainika kujihusisha na vitendo hivyo, wangebanwa ili wataje mbinu zote ambazo huwa zinatumika na kama wapo wengine zaidi nao watajwe waunganishwe katika kundi hilo. 
 Udanganyifu katika mitihani ni adui wa elimu ambaye bila kumchukulia hatua madhubuti, anaweza kusababisha madhara makubwa kwa miaka ya mbele ikiwamo nchi kukosa wataalamu bora wa fani mbalimbali.
 
 Ninaeleza hivyo kwa sababu, wanaofanya udanganyifu wa mitihani na kufaulu kwa njia hiyo, hawawezi kufika mbali kielimu, kwani wanapokosa msaada wa udanganyifu si rahisi kufaulu.
 
 Kwa kuwa udanganyifu huo umeshakemewa kwa muda mrefu lakini bado unaendelea, ninadhani hao waliobainika kushirikisha watoto wadogo wa darasa la nne katika mchezo huo, wangebanwa ili uwe mfano kwao na kwa wengine wenye nia ya kufanya uovu huo ili waache.
 
 Watoto kama hao wa darasa la nne hawana wanachokifahamu zaidi ya kupokea kile wanachopewa. Hivyo, wale waliowashirikisha kufanya kitendo hicho ndio wanaotakiwa kuwajibishwa.
 
 Ninaungana na wale wanaosema kuwa elimu ni kama ibada haitaki najisi. Kwa kuwa watoto ni taifa la kesho, waachwe wafanye wenyewe kulingana na jinsi walivyojifunza bila kuongezewa udanganyifu.
 
 Wakizoezwa kufanyiwa au kudanganya, matokeo yake na wao wataiga mtindo huo na kuuona kama sehemu ya maisha yao. Matokeo yake yanaweza kuwa ni kuongeza wadanganyifu kila sekta miaka ya baaadaye.
 
 Mtindo huo katika mitihani usipodhibitiwa, unaweza kusababisha baadhi ya wanafunzi wakapungukiwa ari ya kupenda masomo na kupoteza uzalendo wao kwa taifa lao ambalo ndio wanalotarajia  kulitumikia mara baada ya kuhitimu masomo yao.
 
 Si sahihi kuwapo wanafunzi wanaofaulu kwa udanganyifu na wengine wakiumiza vichwa kwa kutumia akili zao. Ndio maana nikaeleza kuwa mtindo huo unaweza kusababisha wengine wakapunguza ari ya kusoma kwa kuwa wataona hata wakisoma kwa bidii wapo wenzao ambao watafaulu kirahisi kwa udanganyifu bila kuumiza vichwa.