Malumbano, matusi ndani ya CHADEMA yana athari mbaya

Nipashe
Published at 08:05 AM Jan 08 2025
Malumbano, matusi ndani ya CHADEMA yana athari mbaya.
Picha: Mtandao
Malumbano, matusi ndani ya CHADEMA yana athari mbaya.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiko katika maandalizi ya mwisho ya uchaguzi mkuu ngazi ya taifa. Uchaguzi huo unatarajia kuwapata viongozi wakuu na wale wa mabaraza ya vijana (CHAVITA), Wanawake (BAWACHA) na Wazee (BAZECHA).

Hivi sasa wanaowania nafasi hizo wako katika kampeni za mwisho kushawishi wajumbe kuwachagua ili wawaongoze wanachama na wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini. 

Pamoja na mambo hayo kuendelea, mvutano mkubwa unaonekana katika nafasi ya mwenyekiti baada ya mwanasiasa machachari, mwanaharakati na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kutangaza rasmi na kuchukua fomu kuwania nafasi ya mwenyekiti  inayoshikiliwa kwa sasa na Freeman Mbowe. 

Kujitokeza rasmi kwa Lissu  kuwania nafasi hiyo kumeongeza joto na vuguvugu la uchaguzi huo kuwa kubwa hata kusababisha mgawanyiko miongoni mwa wajumbe na viongozi waandamizi wa chama. Wako waliotangaza waziwazi kuwa wanamwunga mkono Lissu  huku wengine wakisema wanasimama na Mbowe katika kinyang’anyiro hicho. 

Tangu vigogo hao kuchukua fomu na kuzirejesha, kumekuwa na mgawanyiko mkubwa miongoni mwa viongozi, wanachama na wafuasi na kuwapo kwa kambi mbili za waziwazi. Pamoja na kuwapo kwa mpasuko huo miongoni mwa wanachama, viongozi na wafuasi, pia kumekuwa na kauli na maneno yenye viashiria vya kukimega chama katika makundi mawili. 

Kila upande umekuwa ukijaribu kutupa maneno ya kejeli dhidi ya upande mwingine. Kambi ya Mbowe, baadhi ya wafuasi wamekuwa wakitoa maneno kama Lissu mropokaji,  ana uroho wa madaraka na ametumwa kukivuruga chama kwa maana ya kwamba ni kibaraka wa serikali na chama tawala. 

Upande wa Lissu nao umekuja na kauli kadhaa kwamba Mbowe anataka kuwa sultani, hana jipya (kwa maana hana mawazo mapya katika uongozi na maendeleo ya chama), mabadiliko ni lazima na pia lazima kuwe na ukomo wa uongozi. Wafuasi wa kambi hiyo wanaamini kwamba Lissu ndiye atakayeleta mabadiliko ndani ya chama hicho, hivyo ni wakati wa Mbowe kukaa pembeni. 

Kwa ujumla, meneno hayo na kejeli ambavyo havina ishara njema ndani ya chama hicho kilichojijengea umaarufu katika medani ya siasa hasa katika mfumo wa vyama vingi. Ni dhahiri kwamba  kwa wachambuzi na wafuatiliaji wa masuala ya siasa, huenda kauli, mivutano na kejeli hizo, yakakisambaratisha chama kama hali itaendelea kuwa hivyo. 

Mwanasiasa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, aliwahi kusema katika siasa hakuna adui wa kudumu waka rafiki wa kudumu. Kwa mantiki hiyo, ni vyema wanasiasa na wafuasi wa kambi hizo mbili zinazovutana wakatambua kuwa kuna maisha baada ya siasa, hivyo waache kutukanana, kukashifiana na kukejeliana. 

Mivutano na kutofautiana kwa hoja ndani ya vyama vya siasa na serikali hata katika jamii havina budi kuwapo lakini si kwa kutengeneza maneno ya uhasama na uadui. Uchaguzi ndani ya CHADEMA utapita lazima maisha yataendelea kuwapo, hivyo si vyema kutengeneza uadui katika muda mfupi kama wahenga wasemavyo usiache mbachao kwa msala upitao.