WATANZANIA wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) sasa wanaweza kufanya maendeleo mbalimbali wakiwa bado nje ya nchi huko ikiwemo kuwekeza na kusaidia familia zao kwa urahisi zaidi.
Hatua hiyo inakuja baada kampuni ya teknolojia ya kifedha inayosimamia programu ya kifedha kwa Waafrika Kuda kupewa leseni ya Mtoa Huduma za Malipo (PSP) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) chini Tanzania.
Hii itawawezesha wana daispora kutuma hela kwa urahisi kwa ajili ya matumizi ya mbalimbali kama vile uwekezaji katika biashara mbalimbali na huduma za kijamii .
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, uhitaji wa kutuma fedha kutoka nje ya nchi unaofanywa na Watanzania wanaoishi ughaibuni unaongezeka kwa kuwa mwaka 2021, kiasi cha fedha zilizotumwa Tanzania kilifikia dola milioni 569.3, ikionyesha umuhimu wa pesa hizo katika kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kuda Technologies, Babs Ogundeyi, amesema kuwa kupata leseni ya PSP Tanzania ni hatua kubwa kwa kampuni hiyo katika kupanua wigo wa bara la Afrika katika uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi na familia kwa ujumla.
Amesema Watanzania wanaoishi nchi kama vile Uingereza, Umoja wa Ulaya, Marekani, na Canada wanaweza kutumia huduma hiyo kwa gharama nafuu kupitia njia mbalimbali za malipo kama vile kadi, pesa kwa njia ya simu, uhamisho wa benki, USSD na EFT kutokana na ukuaji wa teknolojia.
Amesema Tanzania ni soko muhimu katika kuwahudumia watu wanaoshi ughaibuni na kuwaunganisha na familia zao katika upatikanaji wa huduma za kifedha.
“Leseni tuliyopewa na BOT inatuwezesha kutoa huduma za kifedha za uhakika kwa gharama nafuu ili kuwawezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kushiriki katika ujenzi wa Taifa kupitia uwekezaji na maendeleo ya familia zao,” amesema Ogundeyi.
Aidha, amesema upatikanaji wa huduma hii sio muhimu kwa Tanzania tu, bali bara la Afrika kwa ujumla.
“Tumejidhatiti kuwawezesha Watanzania waishio ughaibuni na kusaidia ukuaji wa kiuchumi wa kanda kwa kutoa huduma za kutuma fedha kwa usalama na urahisi, ambazo zinaimarisha ushirikishwaji wa kifedha."amesema.
Amesema ni fahari kwa Kuda kupewa leseni hii inayowezesha katika kuunga mkono ukuaji wa uchumi hapa nchini, kuwasaidia Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwekeza nyumbani na kuimarisha uhusiano nao na ndugu, jamaa na familia zao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED