Katibu Mkuu wa UN Tourism kuitembelea Mafia

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:10 PM Mar 09 2025
Katibu Mkuu wa UN Tourism kuitembelea Mafia
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa UN Tourism kuitembelea Mafia

Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili, ameahidi kutembelea Kisiwa cha Mafia wakati wa Jukwaa la Pili la Kimataifa la Utalii wa Vyakula, ambalo linatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 23 hadi 25 Aprili 2025.

Tanzania ni mwenyeji wa mkutano huo wa kikanda, hatua inayoonesha nafasi yake muhimu katika kukuza utalii wa vyakula na sekta ya utalii kwa ujumla.

Ahadi hiyo imekuja wakati ambapo Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) inaendelea kuipaisha Mafia kimataifa kwa kuitangaza katika majukwaa mbalimbali. Jitihada hizo zilidhihirika zaidi tarehe 6 Machi 2025, wakati Tanzania ilipopata fursa ya kujitangaza katika maonesho makubwa ya Utalii Duniani ya ITB Berlin, yanayofanyika nchini Ujerumani. 

Katika maonesho hayo, Kisiwa cha Mafia kilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyotangazwa kwa msisitizo mkubwa, kutokana na kuwa na vivutio vya kipekee na vya kuvutia kwa watalii.

Hatua hii inaendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania kama moja ya nchi zinazoongoza katika utalii wa kipekee, hususan katika sekta za utalii wa baharini, utalii wa vyakula, na uhifadhi wa mazingira. 

Ziara ya Katibu Mkuu wa UN Tourism inatarajiwa kuongeza zaidi hamasa kwa watalii wa kimataifa kutembelea Kisiwa cha Mafia na maeneo mengine ya kiutalii nchini Tanzania.