Wanawake TANAPA wazindua maadhimisho Siku ya Wanawake hifadhini Ziwa Manyara

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe Jumapili
Published at 11:06 AM Mar 02 2025
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kaskazini TANAPA, Steria Ndaga.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kaskazini TANAPA, Steria Ndaga.

Ikiwa ni kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika Machi 8 mwaka huu mkoani Arusha na kuongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, zaidi ya wanawake 150 wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Kanda ya Kaskazini wamezindua rasmi wiki ya maadhimisho hayo kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.

Wanawake hao waliwasili hifadhini kwa nderemo na vifijo, wakicheza ngoma na kufungua shampeni katika lango kuu la kuingia hifadhi hiyo. Shangwe zao zilivutia watalii wa kike waliokuwa wakitoka Hifadhi ya Ngorongoro, ambao walilazimika kusimamisha magari yao na kuungana nao katika kusherehekea tukio hilo maalum.

Akizungumza wakati wa msafara huo, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kaskazini TANAPA, Steria Ndaga, alisema wanawake hao ni wafanyakazi wa TANAPA kutoka makao makuu na hifadhi mbalimbali, zikiwemo Hifadhi za Mlima Kilimanjaro, Momela, Tarangire, Ziwa Manyara na Mkomazi.

"Tumezindua wiki ya Siku ya Wanawake Duniani kwa kutembelea hifadhi hii kama njia ya kutambua mchango wa wanawake katika ulinzi wa maliasili na wanyamapori nchini," alisema Ndaga.

Aidha, alifafanua kuwa katika wiki hii, wanawake wa TANAPA wamepanga kufanya shughuli mbalimbali kuanzia Machi 1 hadi kilele cha maadhimisho Machi 8. Shughuli hizo zinahusisha mafunzo maalum kutoka kwa wataalamu wa kuboresha ustawi wa kiakili na kitaaluma, kutembelea watu wenye mahitaji maalum na kushiriki nao katika chakula na burudani, pamoja na kushiriki shughuli mbalimbali zitakazoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

Ndaga alieleza kuwa uzinduzi wa maadhimisho hayo ulianza kwa matembezi ya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, ambapo walishiriki katika utalii wa kutembea kwa kamba juu (canopy walk), kupanda boti ndani ya Ziwa Manyara, na kushuhudia mandhari ya kuvutia ya maporomoko ya maji ya Mto Endabash.

"Shughuli hizi za utalii ni sehemu ya jitihada za kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ni mhifadhi namba moja nchini, katika juhudi zake za kutangaza utalii wa Tanzania duniani. Matokeo yake ni ongezeko kubwa la watalii katika hifadhi zetu," alisema.

Aidha, alibainisha kuwa msimu wa utalii wa mwaka huu unatarajiwa kuvutia wageni wengi zaidi, hivyo akahimiza wadau wa sekta hiyo kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya malazi na huduma nyingine muhimu kwa wageni.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, Dk. Yustina Kiwango, alisisitiza umuhimu wa wanawake kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa maliasili na wanyamapori, akisema kuwa sekta ya utalii inachangia takribani asilimia 21 ya pato la taifa kupitia fedha za kigeni.

"Utalii unachangia sehemu kubwa ya uchumi wa taifa, na hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunalinda rasilimali hizi kwa kizazi cha sasa na kijacho," alisema Dk. Kiwango.

Aliwahimiza wanawake kote nchini kujenga utamaduni wa kutembelea hifadhi za taifa kama Ziwa Manyara ili kujionea vivutio vya asili, ikiwa ni pamoja na maporomoko ya maji ya Mto Endabash, Ziwa Manyara lenyewe, na shughuli za utalii wa kupiga kasia na kutembea juu ya miti, ambazo ni za kusisimua na za kipekee.

Katika hitimisho, wanawake wa TANAPA walimshukuru Kamishna wa Uhifadhi kwa kuwapa fursa ya kushiriki katika maadhimisho haya muhimu kwa muda wa siku nane, wakiahidi kuendelea kushirikiana na wenzao katika kuhakikisha uhifadhi wa maliasili unaimarika kwa faida ya taifa.