MARTHA Mwakilasa (60), amewaomba Watanzania kumpatia msaada wa kifedha ili kukidhi nauli ya kumfuata mwanawe, Jane Mushi, ambaye yuko Marekani na sasa anakumbwa na changamoto ya afya ya akili.
Akizungumza katika ofisi za Nipashe, Mikocheni, Dar es Salaam hivi karibuni, amesema aliandika barua Machi 21, mwaka jana, kwenda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhusu mtoto wake.
Mwakilasa ameeleza namna binti yake huyo mwenye umri wa miaka 39 sasa, anavyoishi na kulala mtaa wa Macberry, Dairy Ashford, jijini Huston, kutokana na kushindwa kujitambua kwa kuwa ana changamoto za afya ya akili.
Barua iliyopatiwa Nipashe na kithibitishwa na Wizara hiyo, iliyoandikwa Desemba 13, 2024 yenye kumbukumbu namba QA.119/75401 na kutiwa saini kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara hiyo, Salvatory Mbilinyi, kisha nakala kwenda kwa Mwakilasa (mama wa Jane), imesema:
“Napenda kukutaarifu kuwa Wizara kupitia ubalozi wetu Washington imefanya ufuatiliaji wa taarifa za Jane Mushi ambaye anadaiwa nchini Marekani.
Baada ya ufuatiliaji hụo imebainika kuwa Jane Mushi aliingia nchini Marekani mwaka 2010 kwa ajili ya masomo yake katika Chuo Kikuu cha Oklahama na baadaye kuhamia katika jiji la Huston Texas, alikopata kazi katika Kampuni ya Lifetime Healthy Care Services LLC.
“Aidha, taarifa zinaonesha kuwa, Jane alianza kuugua afya ya akili na kusababisha kushindwa kupanga maisha yake na kupelekea kuanza kulala mitaani.
“Kufuatia changamoto hizo, mwaka 2018 jumuiya ya Wachaga katika Jimbo la Texas kupitia na Mngwamba ambao walijitolea kumwuguza wakati wa ugonjwa wake waliazimia pia kuanza utaratibu wa kumsaidia ili kurudishwa nyumbani na kuungana na familia yake.
“Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa tuliyoipata zoezi la kumrudisha nyumbani lilishindikana kutokana na Jane kutokuwa tayari kurudi nyumbani Tanzania.
“Hali hiyo ilisababisha Jane kutoroka sehemu aliyokuwa na kurudi mitaani huku akionekana zaidi katika maeneo ya parking za Macberry zilizopo mtaa wa Dairy Ashford jijini Huston na mara ya mwisho alionekana eneo hilo Agosti 2024.
“Kwa taarifa hii ni kweli kuwa Jane Mushi bado yupo hai nchini Marekani, ingawa anakabiliwa na changamoto ya afya ya akili, hali inayompelekea kuishi maisha magumu mitaani bila usimamizi wowote wa ndugu wa karibu.
“Wizara kupitia Ubalozi na jumuiya ya Watanzania Texas, zinaendelea kufuatilia suala lake ili kupata taarifa zaidi kuhusu Jane.
Aidha, kutokana na hali ambayo ameonekana kuwa nayo, Wizara inashauri familia kukaa pamoja na kutafuta namna ya kumpeleka mtu moja kwa moja nchini Marekani, ili aweze kushirikiana na jumuiya ya Watanzania jijini Huston Texas, kumpata Jane na kumrudisha nyumbani.
”Kutokana na hali hiyo, Mwakilasa ametoa wito kwa Watanzania nchini kufanikisha kupata Sh. milioni sita kwa ajili ya safari ya kwenda Marekani kumfuata mwanawe.
Fedha hizo pia zitatumika katika nauli ya kwenda na kurudi. “Ninaomba msaada kwa Watanzania wenzangu, binti yangu nimpate hivyo alivyo, mimi ni mjane, huyu ni mtoto wa pili kati ya watatu,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED