Mwenyekiti Wazazi Morogoro atoa wito watoto kupelekwa masomo ya dini

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 09:19 AM Apr 14 2025
Dk Kellen-Rose Rwakatare
Picha: Mpigapicha Wetu
Dk Kellen-Rose Rwakatare

MWENYEKITI wa Umoja wa Wazazi Mkoa wa Morogoro, Dk. Kellen-Rose Rwakatare amewataka wazazi nchini kujenga utamaduni wa kuwapeleka watoto wao kwenye masomo ya dini nyakati za jioni baada ya masomo ya mchana shuleni badala ya kubaki wakizagaa mitaani.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipokabidhi shiilingi milioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa madirisha na milango kwenye Madrasat Taqwa iliyopo msikiti wa Igima uliopo kata ya Mbingu Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro.

Alisema wazazi hawapaswi kuwaacha watoto wao wakizagaa mitaani na kuwa hatarini kukumbwa na majanga mbalimbali ikiwemo ya ubakaji na tabia mbaya kutoka kwa makundi ya wasiokuwa na maadili.

Alisema madrasa au sehemu yoyote ya mafunzo ya dini ni sehemu salama kwa mtoto na yenye utulivu ambayo itasaidia mtoto kujifunza dini na maadili na kukua akiwa bora baadaye kuwa hata kiongozi bora.

Picha mbalimbali wakati Dk Kellen-Rose Rwakatare alipokwenda kuchangia milioni 2.2 ujenzi wa madrasa Taqwa na choo cha msikiti Mlimba mwishoni mwa wiki Wilaya ya Mlimba Mkoa wa Morogoro.


“Nimewiwa kuja kuchangia madirisha na milango ya madrasa hii kwasababu hii ndiyo sehemu sahihi tuayomtengeneza mwanadamu na mtanzania wa kesho, mtoto akipata mafunzo mema na yenye maadili inasaidia kuwa  nchi iliyo salama na upendo, “ alisema Dk Rwakatare ambaye pia ni Mkurugenzi wa shule za St Mary’s International Academy.

Mmoja wa watoto wanaosoma kwenye madrasa hiyo, Ridhiwani Salum alimshukuru Dk Rwakatare kwa msaada huo kwa kuwa utawasaidia kuondokana na changamoto ya bugudha kutoka kwa wapitia njia jirani na eneo hilo.

Alisema madirisha yakiwekwa yatasaidia kuzuia ndege kuingia kwenye chumba hicho na kuwaepusha na changamoto ya wezi, kuku, mbuzi kuingia kupitia madirishani na kuwasumbua wakati wakijifunza.
Picha mbalimbali wakati Dk Kellen-Rose Rwakatare alipokwenda kuchangia milioni 2.2 ujenzi wa madrasa Taqwa na choo cha msikiti Mlimba mwishoni mwa wiki Wilaya ya Mlimba Mkoa wa Morogoro.

Katibu wa msikiti huo, Hamis Nasoro alishukuru kwa msaada huo ambapo aliomba Serikali na wadau wengine kuwakumbuka kama alivyowakumbuka Mkurugenzi huyo kwani bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mikeka mazuria, na silinigibodi.

Nasoro alisema ujenzi wa madrasa hiyo ulienda sanjari na ujenzi wa msikiti huo uliosimamiwa kwa michango ya waumini wenyewe na kugharimu kiasi cha shiligi milioni 15 na kwamba ujenzi huo ulianza 2012 na unaendelea.

Dk Rwakatare pia alikabidhi shilingi milioni 1.2 kwa  Msitiki wa  Masjid Yusuf Mdemu uliopo kata ya Mchome Wilayani Mlimba mkoani hapa aliyoahidi kwa ajili ya ujenzi wa choo.

Aliwataka waumini na wadau wengine kujitokeza kusaidia ujenga kwenye nyumba za ibada kwa sababu hiyo itasadia kufanya nyumba za ibada kuwa kamili na waumini wengi kuweza kuzitumia inavyostahili.

Alisema yeye  ni mzaliwa wa Mchombe  na ameguswa kuchangia ujenzi wa vyoo vya msikiti huo na kuahidi kuendelea kushirikiana na waumini wa msikiti huo katika kukamilisha ujenzi wake.

Imamu Msaidizi wa Msikiti huo, Abasi Abdalah alisema mtu yeyote atakayejenga msitiki kwa ajili ya Mwenyezi Mungu atahesabiwa mema  na kwamba alichofanya Mkurugenzi huyo ni sadaka.

Alisema ujenzi wa choo hicho ulianza mwaka 2022 kwa kutumia sadaka za waumini na mpaka kikamilike kinahitaji si chini ya shilingi Milioni nane.

Alisema choo hicho kina matundu 10  ambapo vitano ni kwaajili ya wanawake na vitano kwa wanaume na kwamba wametenga matundu mengine kwaajili ya watu wenye mahitaji maalum.