Wabunge wapongeza hatua Soko la Kariakoo

By Christina Mwakangale , Nipashe Jumapili
Published at 04:45 PM Apr 13 2025
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akitoa maelezo kwa wabunge
Picha: Mtandao
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akitoa maelezo kwa wabunge

WABUNGE wameipogeza serikali kwa kufanikisha ujenzi na ukarabati wa Soko la Kariakoo, ambalo limeboreshwa na kuwa na viwango vya kimataifa.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Justin Nyamoga, Aprili 12, 2025, Dar es  Salaam, wakati wakikagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo na maandalizi ya kuwarejesha wafanyabiashara.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Justin Nyamoga akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara ya ukaguzi wa Soko la Kariakoo
“Sisi kama Bunge tumekagua na kujionea kazi kubwa ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan aliyetoa shilingi bilioni 28.03 ili kujenga soko jipya na kukarabati lile lililoungua, mradi huu utanufaisha watu wengi,” amesema Nyamoga.
Mwonekano wa juu wa Soko jipya la Kariakoo leo wakati Kamati ya Bunge ya TAMISEMI ilipokagua utekelezaji wa mradi huo ambapo imeridhishwa na jinsi serikali ilivyoboresha mazingira ya kufanya biashara
Nyamoga ameongeza kusema wabunge wameridhishwa na viwango vya ubora na usalama vilivyowekwa katika Soko la Kariakoo, unaolifanya kuwa na taswira ya kimataifa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Festo Dugange, amesema mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2022 umefikia asilimia 98 ukigharimu zaidi ya Sh bilioni 28, utaongeza nafasi za biashara toka 1,662 hadi 1,907.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wakipokea maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa Soko la Kariakoo
Dugange alieleza kuwa lengo la serikali ni kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara katika Soko la Kariakoo, ambalo litafanya kazi kwa muda wa saa 24 kuwa maandalizi yamekamilika.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema soko litafunguliwa hivi karibuni na kwamba Serikali itahakikisha wafanyabiashara wote wenye sifa wanapatiwa maeneo kulingana na sifa zilizoanishwa.

Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu toka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Amani Mafuru akitoa maelezo kwa Wabunge kuhusu miundombinu ya Soko la Kariakoo
Akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya kuwarejesha wafanyabiashara sokoni hapo, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, Ashraph Abdulkarim amesema tayar wafanyabiashara 1,002 kati 1,520 wa kundi la kwanza wamepangiwa maeneo ndani na mfumo wa TAUSI.

Abdulkarim ameongeza kusema, wafanyabiashara 518 kati ya 1,520 wana changamoto mbalimbali ikiwemo 194 kuwa na madeni ya nyuma, 134 hawajaza fomu maalum na 190 hawana namba ya kitambulisho cha Taifa (NIDA) na Namba ya Mlipa Kodi (TIN), hivyo hawajapangiwa maeneo hadi sasa.