Wenye unene kupindukia waongezeka Z’bar

By Rahma Suleiman , Nipashe Jumapili
Published at 01:36 PM Apr 13 2025
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui
Picha: Mtandao
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui

WAZIRI wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema kuna ongezeko la idadi ya watu wenye hali ya unene uliokithiri kutoka asilimia 26 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 30.8 mwaka 2023.

Amesema ongezeko hilo limebainika baada ya wizara hiyo, kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), kufanya utafiti kujua viashiria hatarishi na ufuatiliaji wa hali ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), nchini kwa watu wenye umri wa miaka 18 hadi 69.

Mazrui ameyasema hayo wakati akifunga mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu uliofanyika visiwani Zanzibar.

Mazrui amesema utafiti huo, unafanyika baada ya miaka 10 toka utafiti kama huo ulipofanyika mwaka 2011 kwa Zanzibar na 2012 kwa Tanzania Bara.

Amesema matokeo ya utafiti yanaonesha bado kuna kazi kubwa ya kufanya, ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.

“Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, kiasi cha matumizi ya pombe kimeshuka toka asilimia 29 mwaka 2012 hadi asilimia 20 kwa mwaka 2023, matumizi ya sigara yamepungua kutoka asilimia 14.1 mwaka 2012 hadi asilimia 10.0 mwaka 2023,” amesema Mazrui.

Hata hivyo Mazrui amesema bado ni asilimia 7.6 tu ya watu ndio hutumia kiwango stahiki cha matunda na mboga, asilimia 20 wameripotiwa kuwa na tabia ya kutumia chumvi kwa wingi na asilimia 10.9 hutumia vyakula vilivyosindikwa viwandani.

“Wataalamu na nyote mnaohudhuria mkutano huu pamoja na uwepo wa viashiria hivi hatarishi, bado taarifa hii imeonesha kupungua kwa matatizo ya kisukari kutoka asilimia 9.1 mwaka 2012 hadi asilimia 2.8 kwa mwaka 2023.

“Tatizo la ugonjwa wa shinikizo la damu, pia limepungua kutoka asilimia 26.0 mwaka 2012 hadi asilimia 22.0 mwaka 2023,” amesema.

Waziri huyo imesema bado kumekuwa na changamoto ya watu kutozingatia matibabu ya magonjwa hayo, takwimu zinaonesha kuwa ni mtu mmoja tu kati ya kila watu watano wenye shinikizo la damu, anatumia dawa na kati yao ni asilimia 3.2 tu ndio wameweza kudhibiti ugonjwa.

Amesema idadi hiyo ndogo ya wagonjwa ambao hawapo kwenye dawa na wanaoweza kudhibiti ugonjwa ndio wamekuwa tishio na mara nyingi wengi hufika hospitalini wakiwa tayari wameshapata madhara makubwa na hivyo hutumia gharama kubwa zaidi kwa matibabu.

Amewataka washiriki wa mkutano huo, kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuendeleza tafiti, kuboresha matibabu na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuzuia magonjwa ya moyo na ni lazima kujenga uelewa wa watu kuhusu tabia bora za kiafya, ikiwamo kula vyakula bora, kufanya mazoezi na kuepuka matumizi ya pombe na sigara.