Mfumo wa kielektroniki kurahisisha usajili malalamiko Wazabuni

By Allan Isack , Nipashe Jumapili
Published at 01:36 PM Apr 13 2025
Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA),James Sando, akizungumza na wazabuni na wadau wa ununuzi wa Umma kutoka taasisi za serikali za Kanda ya Kaskazini wakati wa mafunzo ya Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa
PICHA: ALLAN ISACK
Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA),James Sando, akizungumza na wazabuni na wadau wa ununuzi wa Umma kutoka taasisi za serikali za Kanda ya Kaskazini wakati wa mafunzo ya Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa

Wazabuni hapa nchini,hawatalazimika kufunga safari ya kwenda kwenye ofisi za taasisi za ununuzi au Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA),kupeleka malalamiko pamoja na kufuatilia rufaa zao,kwa kuwa mfumo wa kielektroni umewarahisishia kusajili malalamiko yao sehemu waliko.

Teknolojia ya uwasilishaji wa malalamiko na rufaa kwa njia ya kielekroniki itawasaidia wahusika kutokupoteza muda na gharama za kusafiri kufunga safari ya kwenda kwenye taasisi hizo.

 Hayo yalisemwa jana na Katibu Mtendaji wa PPAA,James Sando,wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa umma kutoka taasisi za serikali kwa Kanda ya Kaskazini, kuhusu matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo (NeST),yaliyofanyika jijini Arusha.

“Moduli hii ina faida kadhaa ikiwemo kumsaidia mzabuni  kutolazimika kufika katika ofisi za taasisi nunuzi au za PPAA,kuwasilisha lalamiko au rufaa yake na inapunguza gharama na muda kwa wazabuni kwa kuwa hawatatakiwa kusafiri kwenda kuwasilisha malalamiko au rufaa zao,”. 

 Hata hivyo,alisema moduli hiyo,ina faida nyingine ikiwamo kuongeza uwazi katika mchakato wa ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa kwa kuwa mzabuni aliyewasilisha lalamiko au rufaa ataweza kuona hatua mbalimbali za ushughulikiaji suala lake.

 Aidha alisema moduli hiyo, inafaidi kwa wazabuni,taasisi nunuzi na PPAA, kwa kuwa inarahisisha zoezi la uwasilishaji na ushughulikiwaji wa malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma.

 Pia aliwataka washiriki kujifunza matumizi ya moduli hiyo, ili waweze kuitumia kwa ufasaha na kuisaidia serikali kupata thamani halisi ya fedha.

Alisema serikali chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, kupitia PPAA wameweza kushughulikia mashauri 171 yaliyotokana na michakato mbalimbali ya ununuzi wa umma.

 Alisema kati ya mashauri hayo, PPAA ilizuia utoaji tuzo kwa zabuni 36 kwa wazabuni wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika. 

 “PPAA kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi zinazosimamia ununuzi wa Umma nchini, tumeweza kushiriki katika kutungwa upya kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 na Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2025,”. 

 Meneja wa Usimamizi wa Rufaa na Huduma za Sheria PPAA,Florida Mapunda, alisema  lengo la mafunzo hayo, ni kuwajengea uwezo wadau wa ununuzi wa Umma kuhusu matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo wa NeST.

“Kwa sasa sheria ya ununuzi wa umma imeweka takwa la ulazima wa ununuzi wa umma kufanyika kwa njia ya kieletroniki kupitia mfumo wa NeST,kutokana na takwa hilo, PPAA imejenga moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko katika mfumo wa NeST, ili kuwasaidia wadau wa ununuzi kuwasilisha malalamiko na rufaa kieletroniki pia,” . 

 Meneja huyo wa usimamizi wa rufaa,alisema moduli imerahisisha zoezi la uwasilishaji wa malalamiko yatokanayo na michakato ya ununuzi wa umma pamoja na kusaidia utunzaji wa kumbukumbu za taarifa za malalamiko na rufaa ambazo zitakuwa zinawasilishwa katika michakato yote ya ununuzi wa umma.