Makalla: waharibu hali ya hewa, fedha majimboni kudhibitiwa

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 02:54 PM Apr 13 2025
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla
Picha: Mtandao
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kupitia utaratibu mpya wa mabadiliko ya katiba yake na kanuni za uchaguzi, wanakwenda kudhibiti wanaojipitisha majimboni kuharibu hali ya hewa wakiwamo wanaojiona wana mfuko mkubwa wa fedha.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla, ameyasema hayo leo, Aprili 13, 2025, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, katika mkutano wa ndani, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku 10 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Makalla anasisitiza kwamba, mabadiliko hayo ndani ya chama yamefanyika kwa njia njema.

“Safari hii hakuna kama mtu umechukua fomu ikiwa mko 100 mtakwenda kupigiwa kura 100 wote, safari hii hapana tutawachuja, mkiwa 100 tutachagua watatu wanaokubalika wakapigiwe kura na wananchi.

“Tumefanya hivyo ili kudhibiti watu ambao wanapita kuharibu hali ya hewa,mbunge yuko kule wanapita,  diwani yuko kwenye mkutano wanapita ili tuwape nafasi madiwani wetu na wabunge kufanya kazi vizuri hadi muda ufike,” amesema.