CHUO Kikuu Shirikishi cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), kimetoa mafunzo maalum kwa walimu 52 kutoka shule ya sekondari ya Mazoezi Chang’ombe kuwapa mbinu mpya mbadala, kutoa adhabu kwa wanafunzi bila athari na kuondoa adhabu kandamizi.
Mafunzo hayo wamepatiwa kupitia Kituo cha Utafiti kuhusu Ulinzi wa Mtoto na kuzuia Ukatili (CPVP) cha DUCE.
Naibu RAS Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi (DUCE) Prof. Amani Lusekelo, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwapa walimu mbinu mpya jinsi ya kutoa adhabu, kuepukana na adhabu kandamizi na kwenda kuwa mabalozi kwa shule zote nchini, kuwapatia mbinu hizo.
Amesema mbinu hizo mbadala zitakwenda kusaidia walimu kuepusha viboko visivyo na utaratibu, kuwabebesha mizigo mikubwa, kuwatukana wao na wazazi wao, kuwapa maneno ya kejeli, kuwadharau na kuwadhalilisha.
Baadhi ya adhabu hizo mbadala, ikiwamo kumpa mwanafunzi adhabu ya kukaa kimya, ahadi, zawadi, kutengeneza urafiki naye, kumpa zawadi za mshtukizo (surprise), kama vile kumfanyia mambo apendayo kama kumpeleka ufukweni, itamfanya mtoto afikirie kwa kina, itamfanya afikirie zaidi mwalimu wangu anataka nini na itamfanya abadilike kitabia.
Amebainisha walimu hao wamesukwa, ili wawe kwenda kuwa mabalozi kwenda kutoa elimu kwa walimu wenzao na wazazi, kwenye shule zingine nchi nzima kuhusiana na mabadiliko ya adhabu shuleni.
“Elimu waliyoipata ni kubwa sana na wanakwenda kuwa mabalozi kwenda kutoa elimu kwa walimu wenzao na kuwapa mbinu kurekebisha mwanafnzi, bila kutumia adhabu kandamizi kwa kutumia maarifa waliyoyapata” amesema
Mhadhiri na Mratibu wa Kituo (CPVP), Dk. Faustine Bwire, amesema ziko njia nzuri sana za kumrekebisha mwanafunzi na kuzuia ukatili, ikiwamo kuwa na ukaribu na kumsikiliza mtoto kwa kina pindi anapokabiliwa na changamoto kutengeneza urafiki.
Pia, kuwashirikisha watoto kwenye mambo muhimu ya kifamilia hususani kumuelekeza mila, desturi na utamaduni pamoja na kuishi vyema na jamii iliyomzunguka.
Kutokupaza sauti kubwa kufoka pindi unapomuelekeza jambo fulani au kumpa katazo ya jambo hilo, na itamjengea urafiki na kumuelewa vizuri mwalimu au mzazi kwa haraka zaidi.
“Walezi na wazazi wengi wanakimbilia matusi na kumfokea kwa sauti mtoto na kumfananisha na wanyama kama vile kumuita mbwa, paka, nguruwe hiyo unazalisha tatizo kubwa la kumfanya huyo mtoto au mwanafunzi awe katili na kumuona adui mwalimu au mzazi na unazalisha vichocheo vya yeye aende kulipiza kwa watu wengine anapoanza kujitegemea,” amesema.
Mwalimu mnufaika wa mafunzo hayo, Tumaini Kasio, amesema wamepata faida kwenye mafunzo hayo na kupata suluhisho jinsi ya kuishi na wanafunzi na watoto na kuacha adhabu kandamizi na kutoa adhabu rafiki na kumbadilisha mwanafnzi.
“Unaingia nae mkataba mwanafunzi unamwambia ukifanikiwa kuacha tabia fulani basi nitakufanyia kitu fulani hapo unakuwa umeshammaliza na atabadilika kwa haraka zaidi,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED