MGOMBEA wa nafasi ya urais kupitia Chama cha National League (NLD), Doyo Doyo, amesema endapo ataingia madarakani ataondoa magari ya kifahari yenye thamani kuanzia Sh. milioni 200 na kuendelea.
Doyo, amesema hayo mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais kupitia chama cha NLD katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba, mwaka huu, amesema serikali yake itatumia zaidi zile ‘Land Rover’ za Sh. million 35 na usafiri wa chini zaidi ya huo.
Aidha, amesema ataondoa pia suala la kuzuia miili hospitalini mpaka ndugu walipe fedha za matibabu, ambazo marehemu hudaiwa kabla umauti haujamkuta.
Amesema suala la kudai fedha kwa ndugu wa marehemu, ili wapewe mwili wakazike ni kosa kubwa hivyo yeye na serikali yake akiingia madarakani ataliondoa na kuongeza atawaachia kama fidia au pole kwa wafiwa.
Amesema atashughulikia pia suala la ajira, ili kuwasaidia vijana wanaomaliza vyuo vikuu na vya kati na kuondoa changamoto ya ajira katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Amesema vipaumbele vyao katika uchaguzi huo ni pamoja na afya, elimu, ajira na miundombinu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED