TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imesema kwamba mpigakura ambaye atakuwa nje ya kituo alichojiandikisha na kutaka kupiga kura, atalazimika kuandika barua kwa Tume siku 40 kabla ya uchaguzi, ili kuruhusiwa kupiga kituo kingine.
Kwa mujibu wa INEC, maombi hayo ya kupiga kura nje ya kituo alichojiandikisha mhusika, yatahusu kura ya Rais pekee, kwamba, mpigakura ataandika barua hiyo kabla ya siku hizo, ili yachakatwe.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima, alisema hayo jana katika mkutano uliofanyika mkoani Dar es Salaam, baina ya Tume hiyo na waandishi wa habari, kuhusu Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Akifafanua zaidi, Kailima alisema mwombaji atapaswa kutaja kituo anachoomba kupigia kura.
Awali, akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, aliwataka waandishi wa habari nchini kutumia taaluma yao kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo na kuwakumbusha kutumia kalamu zao vizuri kwa kuandika habari sahihi.
Aidha, aliwaomba kujiepuka kuchapisha habari zitakazoleta taharuki na kuhatarisha amani ya nchi, badala yake walinde mshikamano ulioko na maadili ya kitaifa.
Jaji Mwambegele alisema waandishi wa habari ni daraja muhimu kati ya Tume na wananchi, hivyo wanayo nafasi ya kipekee ya kusaidia katika kutoa elimu ya mpiga kura, kufikisha taarifa sahihi.
“Tunatambua mchango wenu, mnachangia kwa kiasi kikubwa kuripoti habari za maandalizi, kampeni, upigaji kura na matokeo, hivyo tunaomba mtumie vizuri kalamu zenu katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025,” alisema.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, utoaji wa fomu kwa wagombea wa ubunge na udiwani utaanza Agosti 9 hadi Agosti 27, huku wagombea wa urais na mgombea mwenza ukitarajiwa kuwa kati ya Agosti 14 hadi Agosti 24, huku uteuzi wa wagombea wote ukitarajiwa kufanyika Agosti 27 na kampeni zitaanza kuanzia Agosti 28.
“Katika kipindi hiki cha kampeni, mnapaswa kuhakikisha kuwa vyombo vyenu havitumiwi kuvuruga amani ya nchi. Toeni taarifa za haki, za kweli, na zenye kujenga jamii,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED