Madeleka: Kivule ina matatizo mengi

By Grace Gurisha , Nipashe Jumapili
Published at 05:45 PM Aug 24 2025
Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria kupitia chama cha ACT-Wazalendo,Wakili Peter Madeleka(kushoto) akipokea fomu ya uteuzi kutoka kwa Ally Lugendo, ambaye amekaimu nafasi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria kupitia chama cha ACT-Wazalendo,Wakili Peter Madeleka(kushoto) akipokea fomu ya uteuzi kutoka kwa Ally Lugendo, ambaye amekaimu nafasi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kivule, Peter Madeleka amesema jimbo hilo linakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo matatizo ya miundombinu, elimu, afya, maji, na umeme wa uhakika ndiyo maana chama chake cha ACT Wazalendo kimemteua ili kuondoa changamoto hizo.

Aidha, Madeleka ambae ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania,  amewaomba wananchi wa jimbo hilo wamdhamini kwa idadi kubwa ili aweze kuwawakilisha bungeni  kwa kuonesha kumuunga mkono katika kinyang'anyiro hicho.

Madeleka amesema hayo leo jijini Dar es Salaam, baada ya kuchukua fomu katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ilala, Ukonga, Segerea na Kivule huku akiomba uteuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili aweze kuteuliwa kwenye nafasi ya Ubunge katika jimbo hilo.

"Kupitia uchaguzi wa mwaka huu, tunaamini Tume itatimiza wajibu wake kusimamia uchaguzi ambao utakuwa huru na haki, utaokwenda kuwapa wananchi haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka," amesema Madeleka 

"Kwenye mkoba huu kuna fomu ambazo zinahitaji wadhamini, wanidhamini kwa idadi kubwa sana kwa kuonesha kuniunga mkono katika kinyang'anyiro hicho,"amesema 

Hata hivyo, amesema kupitia Ilani yake ya Uchaguzi inaanisha mambo mbalimbali ya kijamii na kisheria ambayo ndani yake kuna masuala ya haki ambayo wanapaswa kushughulikiwa ipasavyo kwa sababu Serikali ya CCM kwa miaka yote haijawahi kushughulikia ipasavyo. 

"Chama kimeniteua mimi kwa ajili ya kuweza kupeperusha bendela katika uchaguzi, naamini Kampeni zitakapoanza tutapata nafasi ya kutosha ya kueleza ilani ya Chama na mimi binafsi nitaelekezea nimekusudia kufanya nini jimboni,"amesema 

Naye Mvula Emmanuel amesema amechukua fomu kwa ajili kugombea nafasi ya ubunge  katika Jimbo la Segerea katika uchaguzi unaofanyika mwaka huu Oktoba kwa lengo la kuondoa changamoto zinalolikabili jimbo hilo.

"Nazungumza na Wananchi wa Segerea kwamba tunakuja katika kampeni ambazo zitakazotuhakikishia ushindi  ili tuweze kuijenga upya Jimbo letu ambalo CCM kupitia kwa aliyemaliza muda wake kushindwa kufanya chochote," amesema