Miili mingine yapatikana, idadi vifo ajali ya mgodini yaongezeka

By Marco Maduhu , Nipashe Jumapili
Published at 04:39 PM Aug 17 2025
Kikosi cha uokoaji ajali ya mgodi Machimbo ya Nyandolwa wilayani Shinyanga kikiwa na mwili wa Macha Shabani, baada ya kuutoa chini ya ardhi.
Picha: Marco Maduhu
Kikosi cha uokoaji ajali ya mgodi Machimbo ya Nyandolwa wilayani Shinyanga kikiwa na mwili wa Macha Shabani, baada ya kuutoa chini ya ardhi.

KIKOSI cha uokoaji ajali ya mgodi katika machimbo ya Nyandolwa wilayani Shinyanga, kimefanikiwa kutoa miili ya watu wawili, huku idadi ya vifo hadi sasa, ikifikia watu wanne na 18 bado wapo chini ya ardhi.

Miili hiyo imetolewa leo, Agosti 17, 2025. Waliofariki ni Marco Ngelela (26) mkazi wa Sengerema na Macha Shabani (43) mkazi wa Misungwi Mwanza.

Chifu Insepkta Mgodi wa Kikundi cha Wachapakazi Fikiri Mziba, akizungumza kuhusu uokoaji, amesema mchakato unakwenda vizuri na kwamba duara namba 106 wameshatoa watu wote na kusalia duara namba 20 na 103.

Kikosi cha uokoaji ajali ya mgodi Machimbo ya Nyandolwa wilayani Shinyanga kikiwa na mwili wa Macha Shabani, baada ya kuutoa chini ya ardhi
Amesema katika maduara hayo ndani ya siku mbili hadi tatu wanatazamia kumaliza kuwatoa watu wote chini ya ardhi.

Aidha, Agost 11, mwaka huu watu 25 walifukiwa mgodini katika machimbo ya Nyandolwa, wilayani Shinyanga na mpaka leo, kati yao watu saba  wametolewa na 18 bado wapo chini ya kifusi, huku watatu wakiwa hai na wanne wamefariki.