Motisha kwa walimu imeelezwa kuwa chanzo cha Wilaya ya Ludewa kufanya vizuri na kuongoza kwenye ufaulu wa wanafunzi matokeo ya mtihani wa taifa kidato cha sita na kushika nafasi ya kwanza katika wilaya za mkoa wa Njombe.
Hayo yamebainishwa Agosti 23 na Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Ludewa Sunday Deogratias wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu wa shule za msingi na Sekondari iliyofanyika wilayani Ludewa.
Amesema miaka mitatu iliyopita Halmashauri ya wilaya ya Ludewa ilikuwa inashika nafasi ya mwisho kwenye ufaulu wa wanafunzi kwenye mitihani ya taifa kuanzia darasa la saba hadi kidato cha sita.
Amesema baada ya kubaini changamoto ya kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani ya taifa Halmashauri hiyo illianza kutoa motisha kwa walimu na shule ambazo zimefanya vizuri ili waendelee kujituma kazini.
Amesema aliweka utaratibu kwenye Halmashauri hiyo kuwa mwalimu anapofika katika ofisi hizo aanze kuhudumiwa kabla ya wengine ili aweze kurejea kwa wakati katika kituo chake cha kazi na kuendelea na majukumu.
"Mimi mwenyewe nimekuwa mfano wa kusikiliza na kupokea simu za walimu na ofisi yangu muda wote imekuwa wazi kupokea walimu na kuwasikiliza" amesema Deogratias
Amesema kwa kufanya hivyo wamewasogeza karibu walimu wilayani humo na kujisikia fahari kuwa miongoni mwa walimu wa wilaya hiyo na kusaidia kufanya vizuri. Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Ludewa Michael Hadu amesema tangu mwaka 2021 matokeo ya ufaulu wa wanafunzi wilayani humo hayakuwa mazuri na kusababisha kuwa wa mwisho kimkoa.
Amesema katika mitihani ya kidato cha sita mwaka 2023 hadi 2025 wamefanya vizuri kwa kuongoza kimkoa kwa kupata ufaulu wa daraja la kwanza 420 ukilinganisha na mwaka 2021 ambapo walikuwa na ufaulu wa wanafunzi wa daraja la kwanza 38 pekee.
"Mtihani wa taifa wa kidato cha nne tumefaulisha kwa asilimia 98.6 kwa mwaka 2024 na asilimia 98.2 kwa mwaka 2023 kwahiyo tumeendelea kufanya vizuri na ufaulu kupanda siku hadi siku" amesema Hadu.
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Thomas amesema miaka mitatu iliyopita wilaya hiyo ilikuwa inafanya vibaya kwenye mitihani ya taifa kuanzia katika shule za msingi pamoja na sekondari.
Thomas amesema kwa sasa hali imekuwa tofauti kwani wanafunzi wameanza kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya taifa katika shule za msingi na sekondari huko wilayani Ludewa mkoani Njombe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED