KARIBU msomaji wetu tuendelee kuangalia siri za ushindi kwenye maisha yetu. Kila mafanikio ya mtu yana chanzo. Watu wengi walianza kufanikiwa sana, lakini wakashangaa mambo yalipoanza kubadilika ghafla.
Ziko siri za ushindi na baadhi nimeshazijadili. Leo ni mwendelezo wa zilizosalia. Siri nyingine ni kwamba mtu mwenye roho ya hofu, huogopa hata kabla jambo halijatokea.
Hofu ndiyo silaha kubwa sana anayotumia shetani kuwaangamiza wanadamu. Mwenye roho ya hofu hawezi kuchukua hatua yoyote kwenye maisha yake hata kama ana elimu kubwa kiasi gani. Mwenye roho hii huwa anawaza kushindwa wakati hata bado hajajaribu.
Mtu mwenye roho ya hofu ni mtu asiye na imani kwani imani ni kuwa na ujasiri. Mtu muoga ni rahisi sana kupoteza muujiza wake. Roho ya hofu huwa inatengeneza mazingira ili wewe uogope.
Watu wengi wanapoteza miujiza yao kwa ajili ya kuangalia vitisho. Shetani kazi yake ni kukuletea vitisho ili wewe uogope na anajua ukiogopa tu, tayari anakunyang’anya muujiza wako.
Mtu mmoja alisema, mtu mwenye roho ya hofu akipanda kwenye mti, hata kabla hajaanguka anaweka godoro chini ya mti ili akianguka aangukie kwenye godoro.
Hivyo ndivyo watu wenye roho ya hofu walivyo. Hata kabla ya kushindwa, tayari wanaanza kuongea maneno ya kushindwa.
“Eti hivi ikitokea nimeshindwa kurudisha huu mkopo wa benki”. Ushindi unaanza kabla ya kushinda na kushindwa kunaanza kabla ya kushindwa. Hii ina maanisha kwamba kushindwa au kushinda kunategemeana na picha iliyoko kwenye akili yako.
Neno la Mungu linaongea kuhusu hofu pale linaposema, “basi, itakuwa, upanga mnaouogopa utawapata huko, katika nchi ya Misri, nayo njaa mnayoiogopa itawafuatia mbio huko Misri, nanyi mtakufa huko” (Yeremia 42:16). Unachokiogopa ndicho kitakachokuangamiza.
Roho ya mjusi. Ukiangalia kwa nje, “mjusi” ana sura ya kutisha. Ukimwona unachokiwaza ni kwamba ataweza kukudhuru. Lakini inakuwa sivyo. Huyo mjusi anayekutia hofu ukijaribu kumrushia hata kijiti utashangaa atakavyotimua mbio.
Kuna watu wanafanana na mjusi, yaani kwa nje utawadhania ni mameneja wa benki, lakini kumbe hawana hata fedha ya kula. Watu wenye roho hii ya mjusi huwa wana tabia hii; wana uwezo mkubwa sana. Wengine ni wasomi wakubwa lakini wamejaa hofu.
Siku zote wanaogopa kufanya jambo fulani kubwa litakalowaletea mafanikio. Ukiuogopa ukimwi ujue utakuua. Wengi wanapoona akaunti zao za benki zinazidi kupungua pesa wanaanza kuogopa.
Kumbe hiyo ni kuruhusu roho ya kufilisi. Wengi wanaogopa kuhusu kesho, wakati hata hiyo kesho bado haijafika. Hawajui kwamba kesho ipo mikononi mwa Mungu.
Siri nyingine ya ushindi tunayopasa kujua ni kwamba mafanikio ni watu. Ni ukweli kwamba huwezi kufanikiwa kama hauna watu wazuri. Hata kama wewe una upako wa viwango vya juu sana, huwezi kufanikiwa kama huna watu wazuri.
Siri hii wengi hawaijui. Huwezi kuwa milionea, yaani tajiri mkubwa kama hutaweza kutafuta watu watakaokufanyia kazi. Kadiri unavyozidi kuwa na watu wengi waaminifu wanaokufanyia kazi, ndivyo utakavyozidi kufanikiwa kwani watu wengi watakufanyia kazi kubwa zaidi na kuleta mafanikio makubwa zaidi.
Iko kanuni ya upendo. Waajiri wengi, mabosi, hawajui kuishi na wafanyakazi wao vizuri na mwisho wanawapoteza. Jiulize kwa nini unawafukuza wafanyakazi? Ni kweli wako wafanyakazi wazembe wasiofaa. Lakini si wote. Lazima ujue kuishi na watu kunahitaji upendo na uvumilivu.
Ukitaka kuongoza watu vizuri usiogope yatakayotokea, yaani kubali kujihatarisha. Uwe tayari kwa lolote, usiogope kuongeza wafanyakazi kwa kuhofia watakukwaza. Hapo utakosa sifa ya kuwa kiongozi na huwezi kufanikiwa.
Siri nyingine, usiangalie ukubwa wa tatizo, bali angalia ukubwa wa Mungu wako. Mungu ni mkubwa kuliko matatizo yetu. Nguvu zake ni kubwa kuliko matatizo yetu.
Musa alipokutana na tatizo kubwa pale majeshi ya Misri yalipowafuatilia kwa nyuma, na mbele kuna bahari, kulia na kushoto milima, alidhani tatizo hilo ni kubwa kuliko nguvu za Mungu.
Mungu alidhihirisha nguvu zake kuu na bahari ya Shamu ikagawanyika. Watu wa Israeli walipita katikati ya bahari na Mungu akawaangamiza adui zao.
Msomaji wangu, bila shaka umejifunza mengi kuhusu siri hizi. Sehemu ya mwisho wiki ijayo. Ujumbe 0715268581.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED