Dk. Nchimbi: Tutajenga barabara ya Msuya, Stendi ya Mabasi Mwanga

By Gwamaka Alipipi , Nipashe Jumapili
Published at 12:30 PM Sep 14 2025
Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi
PICHA: CCM
Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo kitakamilisha ujenzi wa Barabara ya Msuya (Km 13) pamoja na ujenzi wa Stendi ya Mabasi wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Mgombea Mwenza wa Urais wa chama hicho, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi ametoa ahadi hiyo leo Septemba 14 katika Uwanja wa Msuya, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Vilevile, alisema pia katika miaka mitano ijayo endapo CCM itashinda Uchaguzi Mkuu itahakikisha inaboresha sekta ya elimu ili watoto wilayani humo wanapata elimu bora. Kadhalika, amesema serikali itajenga hospitali, zahanati na vituo vya afya, lengo likiwa ni kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

"Bajeti kubwa inatolewa katika sekta ya kilimo ili mbolea, dawa na mbegu zipatikane kwa wakati kwa bei ya ruzuku. Tunataka tija ya wakulima iimarike siku hadi siku. Barabara zitajengwa za lami na changarawe," alisema Dk. Nchimbi.

Kuhusu sekta ya uvuvi, Dk. Nchimbi amesema serikali ya CCM itaboresha mashamba darasa wilayani Mwanga ili vijana wajifunze kufuga samaki.