Mradi wa TACTIC Mbeya waendeleza miundombinu kwa thamani ya bilioni 51

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 07:33 PM Sep 14 2025
Mradi wa TACTIC Mbeya waendeleza miundombinu kwa thamani ya bilioni 51
Picha: Mpigapicha Wetu
Mradi wa TACTIC Mbeya waendeleza miundombinu kwa thamani ya bilioni 51

Mradi wa Uendelezaji Miji Tanzania (TACTIC) unaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya yenye thamani ya Shilingi bilioni 51, ikihusisha uboreshaji wa miundombinu ya barabara, masoko na stendi za mabasi.

Mratibu wa Mradi wa TACTIC Jiji la Mbeya, Mhandisi Yunus Nsegobya, amesema miradi hiyo inagharamiwa na mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia, ambapo Mbeya ni miongoni mwa majiji yanayonufaika. Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 12.3, taa za barabarani, mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 6.41 na jengo la ofisi la kusimamia mradi kwa gharama ya Shilingi bilioni 21, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 70.

Aidha, miradi mingine inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi katika eneo la Old Airport na Soko Kuu jipya katika eneo la Sokomatola kwa gharama ya Shilingi bilioni 30. Nsegobya alieleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kuongeza mapato ya halmashauri kutoka Shilingi bilioni 24 hadi kufikia kati ya Shilingi bilioni 35 na 40.

Mhandisi Nsegobya ameishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio cha wananchi wa Mbeya kwa kuboresha miundombinu ya msingi, hali iliyoongeza thamani ya jiji hilo na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji. Aliwataka pia wananchi waendelee kulinda miundombinu hiyo ili idumu kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbeya, Mhandisi Boniface Kasambo, alisema baadhi ya barabara zilizokamilika ni pamoja na barabara ya Uyole–Itezi (km 1.8), Ilomba–Machinjioni (km 3.8), Kabwe–Block T (km 1.2), Iziwa (km 2), Kalobe (km 3.8) pamoja na ujenzi wa mfereji wa maji ya mvua wenye urefu wa km 6.41. Alisema barabara hizo zimeleta mabadiliko makubwa kwani sasa wakulima wanasafirisha mazao yao kwa urahisi zaidi kwenda sokoni.

Wananchi nao wameeleza namna walivyonufaika na miradi hiyo. Mkazi wa Mtaa wa VETA–Machinjioni,Victor Mlay, alisema barabara mpya zimeongeza thamani ya maeneo yao, kuchochea biashara na kuboresha huduma za usafiri. Aliongeza kuwa taa za barabarani zitakapowashwa mji utapendeza na biashara zitaendelea hadi usiku.

Naye Mwalimu Ezekia Gwenino wa Shule ya Sekondari Uyole alisema awali barabara zilikuwa na mashimo, matope na vumbi, hali iliyosababisha changamoto ya usafiri kwa walimu na wanafunzi. “Kwa sasa usafiri umekuwa bora zaidi, tunafika shuleni kwa wakati. Nawaomba wananchi wasitupe taka kwenye mitaro ili ibaki katika hali nzuri kwa muda mrefu,” alisema.

Kwa upande mwingine, Zena Nassor, mfanyabiashara katika eneo la Sokomatola, alisema ujenzi wa soko jipya na kubwa utawasaidia kufanya biashara zao katika mazingira bora, huku idadi ya wateja ikitarajiwa kuongezeka mara baada ya kukamilika kwake.