ANITA Mlay ni mwanadada mwenye umri wa miaka 29. Msomi wa Shahada ya Ununuzi na Usimamizi wa Ugavi (Procurement and Logistics). Ni mwenye haiba ya kuvutia, uso wa tabasamu na sasa ni balozi wa matumaini.
Lakini nyuma ya tabasamu hilo pana historia nzito, iliyojaa giza la maumivu ya kihisia, kimwili na kiakili. Anita amewahi kujaribu kujiua si mara moja, si mbili, bali mara tano. Leo hii yupo hai, akisimama hadharani kwa ujasiri kuelimisha jamii kwamba "kujiua kunazuilika."
Anita alitoa ushuhuda wake katika mdahalo maalum ulioandaliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jana kuadhimisha Siku ya Kuzuia Kujiua Duniani (Septemba 10), mdahalo uliohudhuriwa na wataalamu wa afya ya akili, wanajamii na viongozi wa dini.
Katika mazungumzo maalum na Nipashe baada ya mdahalo huo, Anita alifunguka kwa uchungu lakini kwa ujasiri mkubwa kuhusu safari yake ya maumivu iliyoanza tangu akiwa mtoto.
Alisema aliwahi kupitia ukatili wa kijinsia akiwa na umri mdogo, jambo ambalo alilificha kwa miaka mingi kwa hofu, aibu na kukosa mtu wa kumweleza.
"Nilikuwa ninaumia kwa ndani, sikuweza kueleza. Niliamini hakuna mtu anayeweza kunielewa. Nilijiona mzigo, nikaamini njia pekee ya kupata utulivu ni kuondoa uhai wangu mwenyewe," alisema Anita kwa sauti ya kutafakari.
Katika moja ya jaribio lake la kujiua, Anita alieleza jinsi alivyotoka nyumbani bila kuaga, akiwa na dhamira ya mwisho: kufa kwa kunywa sumu. Alienda katika eneo la pagale lisilo na wakazi, aliponunua chipsi na soda ambayo hadi leo hawezi kuivumilia.
"Niliweka sumu kwenye chakula, nikala. Nilikuwa nimejipanga, nilijua nitaondoka kimya kimya. Lakini bahati nzuri, gari lilifika pale likamwaga mchanga, watu wakaniona wakanikimbiza hospitalini," alisimulia.
Alisema alipelekwa Hospitali ya Palestina na kupewa rufani kwa uangalizi zaidi. Ingawa alinusurika kimwili, Anita anasema bado hakupona kiakili. Aliendelea kupata matibabu, huku akiwa anapelekwa kwenye nyumba za ibada kwa ajili ya maombezi, lakini hali ya huzuni ya ndani iliendelea kumtafuna.
Anita anasimulia kuwa baada ya jaribio lake la mwisho, hali yake ya kiafya ilizorota na alifanyiwa upasuaji wa tumbo. Madaktari waligundua kuwa hisia kali na msongo wa mawazo vilianza kuathiri mwili wake kwa njia ya magonjwa.
"Niliteseka sana. Lakini baada ya kupata tiba sahihi ya afya ya akili, nilianza kupata nafuu. Ndipo nikajua kwamba kuna tiba, kuna msaada, na maisha yanaweza kuwa bora tena," alisema.
Leo Anita ni manusura, si tu wa kujiua, bali pia wa ukimya unaotawala suala hili. Ameamua kuwa balozi wa mabadiliko, kutoa elimu, kutia moyo kwa wale walio katika hali alizopitia, na kupaza sauti kwa jamii isibaki kimya.
"Kila ninaposikia mtu amekufa kwa kujiua, moyo wangu huuma. Ninajua mtu huyo alikufa kwa kukosa msaada, kwa kuhukumiwa badala ya kueleweka. Ndiyo maana nimesimama kusema ukweli wangu," alisema kwa msisitizo.
Anita alitoa wito kwa jamii, hasa familia, kuwa karibu na vijana wao, kusikiliza zaidi kuliko kuhukumu. Pia anawahimiza vijana kuongea wazi wanapopitia changamoto, na kutafuta msaada badala ya kufunga moyo na kuishi kwenye giza.
"Kama jamii, tunapaswa kujifunza kusikiliza zaidi. Kusema shida si udhaifu. Na wale wanaopitia maumivu kama niliyopitia, ninawaambia: usijitoe uhai. Kuna msaada. Kuna maisha baada ya maumivu," alisema kwa msisitizo.
Simulizi kama hizi bado ni nadra kusikika wazi katika jamii nyingi. Si kwa sababu hazipo, bali kwa sababu zimezibwa na ukimya, unyanyapaa, hofu na adhabu.
Hayo ndiyo yaliyojadiliwa kwa kina katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Kujiua yaliyofanyika MNH jana.
Kaulimbiu ya mwaka huu, "Tubadili Mitazamo – Kujiua Kunazuilika", iliweka msisitizo si tu kwenye huduma za afya, bali pia kwenye maadili, sheria, uelewa wa jamii na wajibu wa pamoja wa kulinda maisha ya kila mtu.
KIFO SEKUNDE 40
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk. Delilah Kimambo, alieleza kwa uchungu hali halisi inayokumba dunia:
"Kila baada ya sekunde 40, mtu mmoja anajiua. Takribani watu 720,000 hufariki dunia kila mwaka kwa kujiua, na asilimia 90 ya matukio haya yanatokana na matatizo ya afya ya akili."
Dk. Delilah alisema MNH hupokea manusura wa kujiua mara kwa mara na kuwapa huduma za kiafya, lakini jamii haijafikia hatua ya kufahamu na kukubali kuwa matatizo ya kiakili ni halisi na yanahitaji msaada, si hukumu.
Katika mdahalo uliofuatia, ulioshirikisha wataalamu wa afya, viongozi wa dini, wanasheria na wanajamii, walikubaliana kuwa tatizo kubwa si tu idadi ya watu wanaojiua, bali jinsi jamii inavyokabiliana na changamoto hizo.
Dk. Saidi Kuganda, bingwa wa magonjwa ya akili MNH, aliweka bayana kuwa: "Unapomwona mtu anashindwa kuzungumza, amekaa kimya, ameandika ujumbe wa kuaga au kusema ‘mimi nikifa msinisumbue’, hiyo si lelemama. Ni dalili. Tusipuuze."
KOSA LA JINAI
Mkuu wa Kitengo cha Sheria MNH, Veronica Hellar, alieleza kuwa sheria ya sasa inaeleza kuwa jaribio la kujiua ni kosa la jinai linaloadhibiwa kwa kifungo kisichopungua miaka mitano.
"Kumsaidia mtu kujiua ni kosa la kifungo cha maisha. Lakini je, hii inasaidia au inazidisha maumivu kwa manusura?” alihoji.
Kauli yake ilisisitizwa na Faraja Chiwanga, mwakilishi wa jamii, aliyesema: "Kwa muda mrefu waliojiua au walionusurika, wamekuwa wakitengwa hata katika ibada za mazishi. Ni wakati wa kubadilika. Mtu huyu alihitaji msaada, si hukumu."
Usu Mallya, kutoka kundi la viongozi wa imani, alisema unyanyapaa dhidi ya manusura unapaswa kuondolewa mara moja.
"Familia huishi kwa aibu. Manusura huogopa kujieleza. Hii inaficha chanzo halisi cha tatizo," alisema.
DALILI ZA KUJIUA
Dk. Nuruel Kitomary alisisitiza kuwa dalili za mtu anayekaribia kujiua huwa wazi au zilizojificha, na wengi huzipuuzia.
"Mtu anapojiona ni mzigo kwa familia, akianza kujitenga, kuwa mchafu ghafla, au kuandika ujumbe wa kuaga, hiyo ni sauti ya ndani ya kukata tamaa," alitahadharisha.
Alihimiza jamii kuanzisha mazungumzo ya wazi kuhusu afya ya akili na kujenga mazingira rafiki ya kusaidiana, badala ya kuogopa au kumtenga mtu anayepitia hali hiyo.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Mugisha Nkoronko, alieleza utafiti wake ulioonesha watumishi wa sekta ya afya wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kujiua.
"Wauguzi wako katika hatari kwa asilimia 60, wakifuatiwa na madaktari. Hii ni kwa sababu ya mazingira ya kazi, uchovu, msongo na kushuhudia maumivu kila siku," alisema.
Aliongeza kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 39 ndio wanaoongoza kwa kujiua nchini, huku jiji la Dar es Salaam likiongoza kitaifa.
Maulid Nditi kutoka taasisi ya Elimu Khayriya, alihitimisha, akisema: "Tusianze na hukumu. Tuanzie na sababu. Tumwulize mtu ‘unaendeleaje?’ kwa nia ya kumsikiliza na kumsaidia."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED