Othman Masoud Othman: Zanzibar inahitaji uwajibikaji na mwongozo wa kweli

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 02:39 PM Sep 14 2025
Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman
PICHA: MTANDAO
Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman

Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amewahimiza wananchi wa Zanzibar kuchagua viongozi jasiri watakaorudisha hadhi na haki za taifa.

Amesema uwajibikaji umepotea na ufisadi umeenea katika kila sekta. Viwanja vilivyotengenezwa, masoko na miradi ya serikali sasa vinaonekana kuwa vimeshika mkono kwa ufisadi, huku wananchi wakiteseka bila msaada.

Othman amesema, akichaguliwa kuwa Rais, kila aliyefanya makosa atachukuliwa hatua stahiki, na Zanzibar itakuwa na mfumo wa uwazi na usimamizi thabiti.Mgombea huyo amesisitiza kuwa uchaguzi huu sio wa kisiasa tu, bali ni kuchagua kati ya uwajibikaji na ufisadi, kati ya maendeleo halisi na umasikini unaoendelea. Amesema viwango vya makampuni yanayojisajili bara na kufanya kazi Zanzibar bila kulipa kodi vinapoteza heshima ya taifa.

Othman amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi, akisisitiza kuwa Zanzibar inastahili viongozi wenye ujasiri, uwajibikaji na uthubutu, ambao watapambana bila kuchoka kwa maslahi ya wananchi na vizazi vijavyo.

Mgombea huyo amesema kuwa Serikali yake itahakikisha uwajibikaji kamili, mifumo bora ya utaratibu, na mfumo wa uwazi wa kupiga kura, ili kila Mzanzibari apate haki yake bila kunyanyaswa.

Amesema utawala wake utahakikisha unaleta Katiba mpya ya Zanzibar, ili mifumo yote iwe chini ya uwajibikaji, kuondoa changamoto ambazo zimebaki kwa miaka 60 huku wananchi wakiteseka bila suluhisho.

Aidha, Othman amesisitiza kuwa Zanzibar kwa udogo wake haipaswi kumuona mwananchi wake akishindwa kupata chakula cha kila siku, huku njaa ikizidiwa na ubinafsi wa viongozi waliopo madarakani. Amesema hatua zake zote zitaelekezwa kuhakikisha kila Mzanzibari ana maisha bora, usalama wa chakula na fursa za maendeleo.

Othman amehitimisha kwa kusema kuwa sasa ni wakati wa Zanzibar kuchagua viongozi wa kweli, waadilifu, na wenye mapenzi ya taifa, ili kuondoa ufisadi, kurudisha hadhi ya taifa, na kuleta maendeleo yanayoonekana kwa kila Mzanzibari.