Doyo: Serikali yangu italipa fidia kwa waathirika wa Tembo, Kiteto

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 12:11 PM Sep 14 2025
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo,
PICHA: MTANDAO
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo,

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, amesema akichaguliwa atajenga hospitali ya kisasa katika vijiji vya Kijungu na Pori kwa Pori, vilivyopo Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma bora za afya.

Doyo ameyasema hayo leo wakati akiwahutubua wananchi wa eneo hilo ambapo amesisitiza wakazi  hao hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya, aidha kuelekea Kiteto Mjini au Songe katika Wilaya ya Kilindi, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao, hasa katika hali za dharura.

“Nafahamu mnakabiliwa na changamoto nyingi, lakini changamoto ya afya inabeba msingi muhimu katika ujenzi wa taifa. “Ili tujenge taifa imara, tunahitaji wananchi wenye uhakika wa huduma za afya. Kuna haja ya kujenga hospitali hapa ili msilazimike kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu,” amesema Doyo .

Akiwa katika mkutano mwingine na wananchi wa Kiteto Mjini,  Doyo alizungumzia changamoto ya migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, akisema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakitoa taarifa zisizo sahihi huku wakiwazusishia viongozi tuhuma ambazo si sahihi na hazina msingi.

“Wakati mwingine wananchi wanakuwa waongo wanapotoa taarifa na kuwatuhumu viongozi, jambo ambalo si sahihi. Nikiwa Rais, nitatoa maagizo ya kuhamisha staafu yote iliyopo sasa na kuleta mpya Kiteto ili tuone mambo yanavyokwenda, na kuhakikisha tunapata ukweli na usahihi wa taarifa zenu,” amesema Doyo.

Aidha, ameahidi kuweka askari wa wanyamapori katika maeneo ya makazi ya watu ili kudhibiti tembo wanaovamia mashamba na kusababisha madhara makubwa kwa wananchi. Doyo pia ameahidi kuunda tume maalum itakayotengeneza ramani ya maeneo ya wakulima na wafugaji kwa kuweka mipaka ya haki kwa pande zote.

 Amesisitiza kuwa ulinzi shirikishi utaimarishwa ili kuzuia migogoro ya mara kwa mara, na akaonya kuwa serikali yake haitavumilia kundi lolote litakalokiuka makubaliano ya vikao vya kimila au serikali.

Kwa upande mwingine, aliwahakikishia wananchi wote walioathiriwa na uvamizi wa tembo kuwa watapatiwa fidia stahiki kama kifuta jasho kutokana na madhara hayo. Msafara wa kampeni wa mgombea huyo unaendelea na ziara zake kutoka kijiji kimoja hadi kingine. Baada ya kumaliza ziara ya Kiteto, msafara huo umeelekea Wilaya ya Babati.