Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na reli iliyoko kwenye matengenezo, zimetajwa na mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, kuwa zitachochea shughuli za biashara na usafirishaji mizigo na kuufungua kiuchumi Mkoa wa Kigoma, unaopakana na nchi ya Burundi pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo.
Ametoa kauli hiyo leo, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kigoma Mjini na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi. Samia amesema kwa upande wa reli, Kigoma ni muhimu ambapo ujenzi wa SGR unaendelea kwa awamu, akibainisha sehemu ya kwanza na ya pili imekamilika, na zilizobaki sehemu ya tatu hadi tano Mwanza- Isaka kukamilika 2025 na ya Tabora -Kigoma na Uvinza-Msagati kazi zinaendelea.
Amesema uboreshaji huo unakwenda sambamba na reli iliyoko, ambapo vichwa vitatu vya treni hiyo, mabehewa mapya 22 ya abiria na mabehewa 44 ya mizigo yamenunuliwa
“Jumla ya mabehewa 350 ya mizigo na 33 ya abiria yanakarabatiwa, mengi yamekamilika. Kazi inafanywa kwa kushirikiana na wabia wetu ambao wamekarabati mabehewa 60 na mengine manane ya kutunza baridi ili kusafirisha matunda na mbogamboga,” amesema.
Amesema wameboresha kanuni kuhusu waendeshaji huduma, kuruhusu sekta binafsi kufanya biashara, hivyo wale watakaoendana nao watawaruhusu, ili kuleta ufanisi wa usafirishaji mizigo na abiria kupitia SGR na reli iliyoko kwenye matengenezo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED