Wanawake wazidi kuvutiwa kusomea ubunifu majengo

By Beatrice Moses , Nipashe Jumapili
Published at 12:03 PM Sep 14 2025
Wanawake wazidi kuvutiwa kusomea ubunifu majengo
PICHA: BEATRICE MOSES
Wanawake wazidi kuvutiwa kusomea ubunifu majengo

WANAWAKE wameendelea kuhamasika kujitokeza kusomea taaluma ya ubunifu wa majengo na ukadiriaji wa majengo, hatua ambayo inatajwa kufikiwa baada ya hamasa iliyofanywa kwenye shule kadhaa za sekondari nchini.

Hayo yameelezwa na Profesa Geraldine Kikwasi kutoka shule ya Usanifu wa majenzi Uchumi na Managmenti katika Chuo cha Ardhi, wakati wa kwenye Mahafadi ya pili ya wataalam 170 waliokidhi vigezo vya usajili Oktoba 2024 na Mei 2025 chini ya Bodi ya Usajili Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi(AQRB).

“Hali imekuwa tofauti tunaona mafanikio ya hamasa tuliyoifanya, awali taaluma hii ilikwepwa na wasichana lakini sasa wanajiunga hadi  imefikia asilimia 40 ya wanaojiunga kwenye fani hii ni wanawake, haya ni mafanikio kwa kuwa  mwaka 1993 nilikuwa mwanafunzi pekee wa kike kwenye darasa,” alisema. 

Mmoja wa wahitimu hao mkadiriaji majenzi upande wa umeme Rebeka Steven anasema kuwa awali fani hiyo haikutambulika kwa wasichana  lakini sasa inatambulika na inavutia japo mazingira ya kazi yanakuwa ni changamoto kwao bado ni kazi nzuri. 

“Kuna wakati unakwenda kwenye mazingira magumu ya kazi mfano kwenye kusimika nguzo napambana hivyo hivyo,kwa kuwa ni kazi ambayo naipenda ina maslahi ya wastani, tunasisitizwa kujali kazi kwanza maslahi baadaye.” Anasema Rebeka 

Mkurugenzi Msajiliw a Maendeleo ya taaluma, Bundara Robert katika taarifa aliyoitoa ya AQRB alisema mojawapo ya kazi muhimu ya mkandiriaji majengo ni pamoja na kukadiria gharama halisi, hivyo amewataka wataalam hao wapya kuwa mabalozi wazuri wa kitaaluma.   

Alisema taaluma ya wabunifu wa majengo inasomewa kwa miaka mitano baada ya hapo atatakiwa kufanya mafunzo ya vitendo kwa miaka miwili. Mkadiriaji majenzi wao husoma kwa miaka minne na mafunzo ya vitendo ni miaka miwili.