CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Handeni, mkoani Tanga, kimeweka wazi majina ya wagombea wao wa udiwani waliopitishwa na vikao vya juu huku mwandishi wa habari na mdau wa maendeleo wilayani humo, Kambi Mbwana, akifanikiwa kupenya kugombea udiwani katika Kata ya Kwamatuku.
Katika mchakato wa kura za maoni zilizofanyika Agosti 4, 2025, Mbwana aliibuka mshindi kwa kupata kura 439, huku mpinzani wake Mustafa Beleko aliyekuwa anawania nafasi hiyo kwa kipindi cha nne akiambulia kura 207, wakati mshindi wa tatu Joseph Minango akiambulia kura saba.
Vikao vya mwisho vya uteuzi katika ngazi ya mikoa kwa madiwani vilikamilika Agosti 13, 2025 tayari kwa wagombea hao kuwania nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu, tayari mgombea wa urais, Dk. Samia Suluhu Hassan, akiwa ameshachukua fomu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Akizungumza mara baada ya kupata taarifa za kupitishwa kama mgombea udiwani wa kata hiyo, Mbwana amesema anamshukuru Mungu kwa kupitishwa na vikao vya chama na kumthibitisha yeye kuwania nafasi hiyo ya kuwawakilisha wananchi.
"Namshukuru Mungu jina langu limepenya mbele ya vikao vya uteuzi. Zilikuwa ni siku ngumu tangu tulipochukua fomu, tulivyochujwa na baadae kufikishwa kwa wajumbe na hatimaye kupata kura nyingi za wenye chama chao," amesema Mbwana.
Joto la uteuzi kwa sasa limebakia katika nafasi za ubunge, kikao cha Kamati Kuu Taifa kitakachokaliwa Agosti 20, mwaka huu, ndicho cha mwisho kinachosubiriwa kutoa majina ya wanachama watakaopewa nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM katika majimbo mbalimbali nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED