MGOMBEA wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, jana amechukua fomu ya kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, mwaka huu.
Baada ya kuchukua fomu hiyo jana, mkoani humo, ametafsiri hatua hiyo kama mwendelezo wa safari ya kufanya mageuzi makubwa kwenye miaka mitano ijayo na kujenga kesho iliyobora kwa kila mwananchi.
Samia ambaye aliambatana na mgombea mwenza, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, katika mchakato huo, aliwasili jana katika Ofisi za INEC majira ya saa 11:15 asubuhi, akisindikizwa na msafara wa viongozi na wanachama wa CCM waliokuwa na shamrashamra, mabango na nyimbo za kumnadi nje ya ofisi hizo.
Akizungumza katika hafla ya mapokezi ya wagombea hao, Makao Makuu ya CCM, mgombea Samia alisema mbio za kuelekea Oktoba zimeanza rasmi.
“Kama ni mpira filimbi imepulizwa, mchezo unakwenda kuanza ikifika Agosti 28, 2025, tutafungua rasmi kampeni zetu na ikifika Oktoba 28, tunamaliza rasmi kampeni zetu na tunakwenda kusikiliza wananchi wanatuambiaje.
“Wahenga walisema ukitaka uhondo wa ngoma ingia ndani ucheze, sasa CCM tumeingia rasmi na tuko tayari kudemka jinsi ngoma itakavyopigwa, tuko tayari kucheza na kudemka.”
Alishukuru CCM kwa imani kubwa waliyoonesha kwake na mgombea mwenza kuwania nafasi hiyo.
ANAYOJIVUNIA
“Serikali ya CCM imefanya mambo makubwa tena katika sekta zote katika kipindi cha mwaka 2021-2025. Hakuna sekta ambayo hatukuigusa, mafanikio hayo yako dhahiri.
“Niwahakikishie kwamba katika miaka mitano ijayo tunapokwenda kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, tutafanya mambo makubwa zaidi,”aliahidi.
Alisema safari ya kufanya mambo hayo itaanza rasmi Agosti 28, mwaka huu, kwa kupita na kuwaeleza wananchi na kuomba ridhaa yao.
“Hii si safari yangu na Mgombea Mwenza peke yetu, bali ni safari ya kila Mtanzania na ndio maana katika utaratibu wa kidemokrasia kila baada ya miaka mitano vyama vya siasa tunarudi kwa wananchi kutafuta ridhaa yao, ili kupata nguvu kuendesha serikali baada ya uchaguzi,” alisema.
Aidha, alieleza kuwa katika safari hiyo, Watanzania wanakwenda kuchagua chama wanachoona kitawaletea maendeleo na kujenga taifa lenye ustawi kwa wote na lenye utu, haki na usawa, uchumi imara unaoelekea kujitegemea.
“Niwaulize ndugu zangu, wengine wataweza kufanya haya? Hii ni safari ya kwenda kuwaeleza wananchi, sera za kila chama katika kuhakikisha tunajenga kesho iliyobora kwa kila mwananchi na kwa vizazi vya sasa na vijavyo na vinavyokuja.
CCM IMEJITOSHELEZA
“Kwa upande wetu CCM yale tunayokwenda kuyafanya, tumebainisha katika Ilani ya Uchaguzi 2025-2030 na yanakwenda sambamba na malengo yetu ya Dira 2050, ambayo ni kuimarisha uchumi wa viwanda, ubunifu kilimo cha kisasa, ajira kwa vijana na wanawake na afya bora kwa wote,” alisema.
Alisema katika kuyatekeleza hayo, serikali inayowekwa na CCM ina uzoefu mkubwa katika kutekeleza.
“Sisi si wanafunzi hata kidogo wengine wote wanajifunza kuanza, lakini sisi ni wazoefu wa kufanya haya, wakati muafaka utakapofika tutapita kote nchini kueleza wananchi yale ambayo tunakwenda kuyafanya, ili nao wakatupe ridhaa yao ya kwenda kuyatekeleza,”alisema.
AOMBA UDHAMINI
Samia alisema wamechukua fomu hiyo na kwamba, bado haijakamilika na ili ikamilike wanapaswa kujitokeza wanachama wamdhamini wa mgombea.
“Fomu hii sasa itapelekwa mikoa yote nikiomba kupata wadhamini wanaotakiwa kwa mujibu wa sheria. Niwaombe mjitokeze kwa wingi wakati fomu hii itakapofika mikoani mwetu kuomba wadhamini,” alisema.
MAKUNDI UBUNGE,UDIWANI
Mgombea huyo alisema ndani ya siku chache zijazo wagombea wote CCM itakamilisha mchakato wa uteuzi wao wa ubunge na udiwani watakaokwenda kushindana na wagombea wa vyama vingine.
“Niwaombe sana, wanachama wote, kama ilivyo desturi yetu kwa CCM mchakato wa uteuzi unapoisha na makundi nayo yaishe na ushindani ndani ya chama uishe.
“Turudi kuwa kitu kimoja ili tuingie katika Uchaguzi Mkuu CCM kukiwa na chama madhubuti chenye umoja na mshikamano,” alisema.
Aliwaomba kudumisha umoja na kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono wagombea wa CCM wanapokwenda INEC kuchukua fomu za kugombea, ili kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM.
Alisema wamekuwa wakipokea fedha kutoka makundi mbalimbali kwa ajili ya fomu hiyo na wamelipia fomu jana.
NCHIMBI: SITAKUWA MSHINDANI WAKO
Balozi Nchimbi, alimshukuru Samia kwa kumpendekeza kwenye Kamati Kuu ya CCM ili kuwa mgombea mwenza na kamati hiyo kwa kuunga mkono pendekezo hilo.
“Ninashukuru Mkutano Mkuu wa CCM kwa kunithibitisha. Nitumie nafasi hii kukuhakikishia wewe, chama na wana-CCM niko tayari kuungana na wewe katika kukitafutia ushindi wa kishindo chama chetu nchi nzima. Nikuhakikishie nimejiandaa kikamilifu huku nikijua chama chetu kina ushindi wa kishindo nje.
“Nimejiandaa kikamilifu kuwa msaidizi wako na sio mshindani wako. Nitakusaidia kwa nguvu zangu zote kwa uwezo wangu wote, ili uweze kutekeleza Ilani ya CCM na kutengeneza historia ya kipekee kwa chama chetu ambayo haijapata kutokea,”alisema.
SILAHA ZITAKAZOTUMIKA
Awali, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wassira, alisema hatua ya mgombea huyo kuchukua fomu ni utekelezaji wa wa azimio la Mkutano Mkuu wa CCM ulifanyika mwezi Januari, Mwaka huu, ambao ndio uliomteua kwa asilimia 100 kuwa mgombea wa urais na ni mwanzo wa kuanza kazi ya kuinadi Ilani ya CCM.
“Wito wangu kwa wanachama, tumeanza safari na mitambo iko sawa kabisa, tumei- test (kujaribu) na inafanyakazi, na tarehe 29, mwezi huu, baada ya kukamilisha taratibu za kisheria la kutimiza matakwa ya kisheria, tuaanza kazi ya kampeni rasmi na kwa muda wa siku 60 mitambo itakwenda kila mahali.
“Ninataka niwaambie Watanzania na wapenzi wetu, tunasilaha mbili ambazo tutazitumia katika kazi hii. Moja ni mafanikio makubwa ya kihistoria yaliyopatikana katika utekelezaji wa Ilani iliyopita na silaha ya pili ni Ilani yetu iliyosheheni mambo mengi.
“Wanachana hakuna cha kuhofu , hata wakiwa 100 kwasababu katika safari na kenge wapo, lamgambo limelia safari imeanza,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu (CCM-Tanzania Bara), John Mongella, alisema CCM imejiandaa vizuri kimuundo, kiuongozi na kimkakati, ili kushinda kwa kishindo Uchaguzi Mkuu 2025, katika nafasi ya urais, wabunge na madiwani.
“Hatua za wabunge, uwakilishi na madiwani ambao utakamilishwa Agosti 20, mwaka huu, ambapo chama kitatangaza wagombea wake kwa nafasi hizo.
ILIVYOKUWA INEC
Samia aliwasili saa 11:15 asubuhi INEC ukiongozwa na msafara na pikipiki za CCM pamoja na viongozi wa chama na serikali na kupokewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Kailima Ramadhan, na kuingia katika ofisi za kutolewa fomu na kukabidhiwa na Mwenyekiti wa INEC, Jaji (Rufaa), Jacobs Mwambegele.
Akitoa maelezo kabla ya kukabidhi fomu, Jaji Mwambegele alisema kwa kuzingatia matakwa ya Katiba na Sheria na Kanuni za Uchaguzi anawakabidhi nakala 40 za fomu za uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais, ambayo ni fomu namba 8A.
Pia alisema amekabidhi nakala nane za tamko za mgombea za kuheshimu na kutekeleza kanuni za maadili uchaguzi 2025, ambayo ni fomu namba 10, nakala mbili za Katiba ya Tanzania, nakala mbili za sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba moja ya mwaka 2024, nakala mbili za INEC namba mbili ya mwaka 2024.
“Nakala mbili za kanuni za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani yam waka 2025, nakala mbili, za kanuni ya INEC za mwaka 2024, nakala mbili za kanuni za maadili za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025, nakala mbili za vitabu vya maelekezo kwa vyama vya siasa,” alisema.
Aidha, alisema pamoja na nyaraka hizo, watapatiwa barua yenye kuonesha namba ya akaunti fedha za malio ya dhamana.
“Waheshima mliopendekezwa nafasi ya kiti cha Rais na Makamu wa Rais, tunawasihi mkazisome nyaraka zote tunazowapatia leo (jana), ili ziwasaidie katika ujazaji wa fomu za kuomba kuteuliwa wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais kufanya kampeni na michakato yote ya uchaguzi,”alisema.
Baada ya maelezo hayo, mgombea Samia na Dk. Nchimbi walisaini kupokea fomu hizo walizokabidhiwa na Mwenyekiti wa INEC.
Baada ya kukamilisha mchakato wa kukabidhiwa fomu, wagombea hao walitoka katika ofisi za INEC wakiwa na mkoba maalum wenye rangi nyeusi ulioandikwa ‘Fomu za uteuzi wa wagombea kiti cha Urais na Makamu wa Rais’.
Kabla ya kuondoka katika jengo hilo, wagombea hao wa CCM walipiga picha za kumbukumbu na makundi mbalimbali ikiwamo, wajumbe wa kamati kuu.
Kundi lingine lililopiga picha ni wajumbe wa baraza la wadhamini la CCM, Wenyeviti wa CCM katika mikoa pamoja na Mwenza wa na Mama wa Balozi Nchimbi.
Saa 11: 47 asubuhi msafara wa mgombea wa urais Samia na Dk. Nchimbi uliondoka kuelekea Ofisi za Makao Makuu ya CCM.
ACHANGIWA 250,000/-
Kabla ya kuelekea Ofisi za Tume, Msafara wa Rais Samia ulisimamishwa na wananchi wa Kijiji cha Chamwino saa 10:45 asubuhi, ambapo walimwombea dua maalum kisha kumchangia fedha Sh. 250,000 za kuchukua fomu na walimtakia kheri Samia katika safari yake ya kuwania kiti cha urais.
Akiwasalimia wananchi hao, Mgombea Samia alisema baada ya kuchukua fomu hiyo atairejesha kwa wananchi kwa ajili ya kumdhamini, ili kuanza safari ya kuelekea uchaguzi mkuu.
MAMIA BARABARANI
Wakati msafara huo ukiwa njiani, baadhi ya wananchi na wanachama wa CCM walikuwa wamesimama kando mwa barabara kushuhudia msafara ukipita, huku wengine wakiwapungia mkono wakiwa wameshika bendera za CCM.
Msafara huo ukiwa umesindikizwa na pikipiki zenye rangi ya CCM zikiendeshwa na vijana waliovalia sare za chama hicho tawala, ulipofika eneo la Wimpi katika mzunguko wa barabara mkabala na jengo la Safina ulipokewa na mamia ya wananchi na wanachama wa CCM.
Akiwa katika gari yenye rangi ya kijani, Rais Samia alisimama kuwapungia mkono wananchi waliojipanga kando mwa barabara.
Rais Samia akiwa na mgombea mwenza Balozi Nchimbi msafara wao ulipokewa na maandamano ya baiskeli, matarumbeta, kinamama na vijana wakiimba nyimbo mbalimbali za hamasa.
Msafara huo uliofika usawa wa viwanja vya Nyerere na wagombea walishuka katika magari hayo kuungana na mamia ya wananchi kutembea kwenda katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM.
Msafara wa viongozi hao wakitembea kwa miguu uliingia katika jengo la Makao Makuu ya CCM saa 12:25 mchana na kupokewa na shamrashamra za wanachama wakiongozwa na bendi TOT, vikundi vya hamasa na wasanii.
Imeandikwa na Augusta Njoji na Renatha Msungu, DODOMA
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED