OFISI ya Makamu wa Rais (VPO) kwa kushirikiana na wadau wa mazingira imeanza utekelezaji wa mkakati na Mpango wa Taifa wa Hifadhi ya Bionuai (NBSAP) kwa lengo la kutambua na kusimamia maeneo ambayo hayajapewa hadhi ya kisheria ya hifadhi ili kulinda viumbe hai na mifumo ya ikolojia.
Ofisa Mazingira Mkuu kutoka VPO ,Martha Ngalowera alisema hayo mjini Morogoro kwenye kikao kazi kilichowakutanisha wadau wa mazingira kutoka Mashirika ya Kimataifa likiwemo Shirikisho la Uhifadhi wa Mazingira Asilia na Maliasili Duniani (IUCN).
Ngalowera alisema mpango huo ni pamoja na kuandaa mkakati wa hifadhi ya bioanuai nje ya maeneo rasmi ya hifadhi, maarufu kama OECMs (Other Effective area-based Conservation Measures).
Alisema lengo ni kuhifadhi asilimia 30 ya ardhi ili kurushisha bioanuai zilizopotea ili ziweze kusaidia kujenga mifumo ya ikolojia kwa ustawi wa jamii duniani kuanzia 2025 hadi ifikapo mwaka 2030.
Alitja maeneo yanayopaswa kufikiwa ni pamoja na mashamba ya kijamii yanayosimamiwa na wanajamii kwa , misitu inayolindwa kwa mila na desturi, vyanzo vya maji vinavyosimamamiwa na vijiji ,pamoja na maeneo ya ufugaji wa asili.
Ofisa Mazingira Mkuu kutoka VPO alisema kuwa Dira ya Taifa ya 2050 imeweka wazi malengo na dhamira thabiti za maendeleo ili kujenga Taifa linalo hifadhi na kutumia rasilimali za asili kwa ufanisi.
“ Kwenye Dira ya Taifa iliyozinduliwa hivi karibuni tunahitaji kufikia malengo ya dira hiyo kupitia uhifadhi wa bioanuai nje ya eneo la hifadhi na inataka Tanzania iwe ni nchi moja wapo kati ya 10 Duniani inayoweza kuhifadhi Bioanuai vizuri “ alisema Ngalowera.
Naye Mratibu wa Uhifadhi Bioanuai kutoka IUCN,Fadhili Njilima alisema Tanzania ni kati ya nchi 12 Duniani zenye utajiri mkubwa wa Bioanuai .
Alisema kuwa unapozungumzia bioanuai ni pamoja na wanyamapori ,aina za makazi ya wanyama ikiwemo milima hifadhi za Taifa , misitu yenye thamani na utajiri pamoja na mapori ya akiba.
Njilima alisema mjumuisho na utajiri wa bioanuai uliopo Tanzania umeyafanya mashirika ya kimataifa ilikiwemo la IUCN yaone kuna umuhimu mkubwa wa kusaidia jitihada za Serikali inazozifanya na hasa ikizingatiwa kuna viumbe wa kipekee ambao wanapatikana Tanzania peke yake .
Alisema licha ya utajiri huo ,yapo matishio mengi yanajitokeza ikiwemo kupungua kwa makazi viumbe hai ambayo yanatokana na upanuzi wa mashamba wa kiholela na usio wa kisheria .
Alitaja eneo lingine ni uvamizi wa maeneo kwa ajili ya uchugaji wa mifugo pamoja na mabadiliko ya tabianchi ambayo ni miongoni mwa sababu kubwa zinazohatarisha bioanuai kuathirika.
Alisema mpaka sasa kuna upotevu wa viumbe hai mbalimbali ambao kwa kiasi kikubwa idadi yao inazidi kushuka na vingine vinazidi kuadimika na baadhi kuelekea kupotea kabisa.
Wadau wa Mashirika mengine walioshiriki mpango huo ni The Nature Conservancy (TNC), Frankfurt Zoological Society (FZS) na Worldwide Fund For Nature (WWF),pamoja na Wataalamu wa Wizara na Taasisi za kisekta kwa ajili ya kukuza uelewa kuhusu utekelezaji wa kuhuisha masuala ya hifadhi ya bioanuai katika mipango yao .
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED