UPDP: Waandishi habari kuwa huru, tutawapa vitendea kazi

By Renatha Msungu , Nipashe Jumapili
Published at 04:22 PM Aug 10 2025
Mgombea urais kupitia Chama cha UPDP, Twalib Kadege
Picha: Ibrahim Joseph
Mgombea urais kupitia Chama cha UPDP, Twalib Kadege

MGOMBEA urais kupitia Chama cha United People Democratic Party (UPDP), Twalib Kadege, amesema moja ya vipaumbele vyao endapo wataingia madarakani, ni kuhakikisha wananchi wote wanapatiwa ardhi pamoja na waandishi wa habari kufanya kazi kwa uhuru na kupatiwa vitendea kazi.

Twalib amesema hayo, mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Amesema suala la ardhi ni kila mtu anapaswa kuwa nayo, ili aweze kuitumia katika mambo mbalimbali, ikiwamo kilimo kwa ajili ya kujiinua kiuchumi wao na familia zao.

Mgombea urais kupitia Chama cha UPDP, Twalib Kadege (kulia) na Mgombea mwenza, Abdalla Mohamed Khamis
"Pamoja na kuwa hatujazindua Ilani yetu, lakini hivyo ndivyo vipaumbele vyetu kwa wananchi pale watakapotupa vifaa," amesema Kadege.

Kuhusu suala la waandishi wa habari, amesema atawawezesha vitendea kazi, ili waweze kwenda vijijini kuandika habari zao kwa uhuru, bila buguza ikiwamo kuruhusiwa kuandika habari zote.