Vyama vyajinoa kampeni uchaguzi

By Beatrice Moses , Nipashe Jumapili
Published at 10:24 AM Aug 26 2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele

MOTO wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 unazidi kuwaka, huku vyama mbalimbali vya siasa nchini vikitangaza tarehe na maeneo ya uzinduzi wa kampeni zao. Kampeni hizo zinatarajiwa kuanza rasmi Agosti 28, yaani katika siku mbili zijazo, ambapo wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani wataanza kuomba ridhaa ya wananchi.

Chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimetangaza kuwa kitaanzisha kampeni zake kwenye Viwanja vya Kawe, Dar es Salaam, siku hiyo hiyo ya uzinduzi wa kitaifa.

Kwa upande mwingine, ACT-Wazalendo kimetangaza kuwa uzinduzi wa kampeni zake utafanyika Agosti 30 kwenye Uwanja wa Furahisha, jijini Mwanza, huku macho ya wengi yakiwa kwa chama hicho kufuatia pingamizi lililowekwa dhidi ya mgombea wake wa urais.

National League for Democracy (NLD) imetangaza kuzindua kampeni Septemba 4 mkoani Tanga, lakini Katibu wake Doyo Hassan amesema wanakabiliwa na changamoto ya kifedha.

"Tulipanga bajeti ya Sh. bilioni tano, lakini hata bilioni moja bado haijapatikana," alisema Doyo.

UPDP imepanga kuanzisha kampeni Septemba 5 kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza, kwa mujibu wa Mwenyekiti wake, Twalib Kageze.

CCK imethibitisha kuwa kampeni zao zitazinduliwa jijini Dar es Salaam, ingawa bado haijathibitisha tarehe rasmi wala eneo.

TLP kupitia Katibu Mkuu wake, Yustus Rwamugira, imesema ratiba ya uzinduzi itatangazwa baada ya mchakato wa uteuzi kukamilika Agosti 27.

ADA-TADEA imetangaza kuwa uzinduzi wake utafanyika Septemba 14 katika Uwanja wa Zakhem, Mbagala mkoani Dar es Salaam.

SAU imesema itaweka mbele uzinduzi wa ilani ya uchaguzi, kisha ifikapo Septemba 7, itazindua kampeni rasmi huko Gongolamboto, jijini Dar es Salaam.

Katibu wa NCCR-Mageuzi, Eveline Munisi, alisema watazindua kampeni tarehe 6 Septemba katika Jimbo la Buhigwe, mkoa wa Kigoma.

DP, NRA na UMD bado wako katika hatua za maandalizi ya ndani na uteuzi, ambapo tarehe rasmi za uzinduzi zinasubiri kupangwa au kuidhinishwa na kamati kuu za vyama hivyo.

HATIMA YA MPINA

Wakati ACT-Wazalendo ikiendelea na maandalizi ya uzinduzi wa kampeni, hali ya sintofahamu imeibuka kuhusu mustakabali wa mgombea wake wa urais, Luhaga Mpina, kufuatia pingamizi lililowasilishwa dhidi yake na Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala.

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nayahoza, amethibitisha kuwa uamuzi wa pingamizi hilo utatolewa wakati wowote kuanzia sasa, baada ya kupitia taarifa zote muhimu.

"Kamati ya Maadili iko kwenye hatua za mwisho za kupitia pingamizi hilo, na taarifa rasmi itatolewa punde," alisema Nayahoza.

Tuhuma dhidi ya Mpina zinahusiana na upungufu wa kimaadili na kiuongozi, jambo ambalo limeibua mijadala mikali kwenye duru za kisiasa na mitandao ya kijamii. 

Wadadisi wa siasa wanaona pingamizi hilo linaweza kuwa na athari kubwa kwa ushindani wa kisiasa iwapo litatolewa uamuzi unaomwondoa katika kinyang’anyiro cha urais.