MIRADI minne ya kimkakati iliyozinduliwa wiki hii na Rais Samia Suluhu Hassan, imetangaza fursa lukuki kwa Watanzania, zikiwamo ajira 273,700 na biashara ndogo na za kati.
Wataalamu wa uchumi wamewataka Watanzania kuchangamkia fursa zilizoko kwenye mnyororo wa thamani wa miradi hiyo, zikiwamo huduma za chakula, makazi, nyumba za wageni, usafirishaji wa watu na bidhaa, na usambazaji wa bidhaa.
Miradi inayotajwa ni ule wa kiwanda cha majaribio cha uchenjuaji madini ya urani, kilichoko wilayani Namtumbo, Ruvuma; bandari kavu ya Kwala na kongani ya viwanda Kibaha, Pwani; na Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC), kilichoko Ubungo, Dar es Salaam.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hii, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini nchini (REPOA), Dk. Donald Mmari, alisema miradi hiyo inakuja na fursa nyingi, na kuwahimiza Watanzania kuzichangamkia.
“Miundombinu (Kwala), inafungua fursa za biashara na kiuchumi, inapunguza gharama za uchukuzi, inachagiza mzunguko wa bidhaa…malazi yatahitajika, chakula, usafiri na makazi,” alisema.
Dk. Mmari alisema kwa upande wa Namtumbo, fursa ni hizo hizo, akiweka msisitizo wa usafirishaji hususani wa madini hayo.
“Uzalishaji utakuwa na wafanyakazi ambao watahitaji vyakula, mafuta na kutakuwa na fursa za kuzaliwa kwa viwanda vingine vidogo,” alisema.
Mtaalamu wa uchumi, Dk. Donat Olomi, alisema: “Hii miradi siyo tu kwamba inazalisha ajira, lakini inachangia katika kuleta mageuzi kwenye uchumi, kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kuchagiza ukuaji wa sekta nyingine.”
Alitoa mfano wa Bandari ya Kwala, akisema itakupunguza gharama za usafirishaji, msongamano barabarani na kuongeza ushindaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
“Mizigo itaingia mingi zaidi, serikali ikaingiza fedha nyingi, kupunguza gharama kutafanya uchumi ukue kwa kasi na inasaidia sekta nyingine nyingi kukua.
“Ukipunguza gharama za usafirishaji, inaleta athari chanya kwenye biashara zingine, viwanda na huduma. Bandari ya Kwala italeta matokeo makubwa kwa nchi,” alisema Dk. Olomi.
Kuhusu mradi wa urani, alisema utaongeza mapato ya fedha za kigeni ambayo yataimarisha thamani ya Shilingi ya Tanzania, kuongeza akiba ya fedha za kigeni na kuzalisha viwanda vingine.
Akichambua mradi wa Ubungo, Dk. Olomi alisema ni eneo la kimkakati ambalo kama litatumiwa vizuri, linaweza kuwa kituo cha mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi katika nchi nyingine za Afrika.
“Watu wenye viwanda vidogo wakitaka kuagiza mitambo wanahangaika kutokana na mchakato mrefu ambao haueleweki; na wakati mwingine anaagiza kifaa kinakuja anakuta kwamba, si alichohitaji, hakina ubora au anatapeliwa.
Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Prof. Samuel Wangwe, alisema mbali ya kuzalisha ajira na kukuza biashara nyingine, miradi hiyo itakuza ujuzi wa teknolojia kwa Watanzania watakaofanyakazi humo.
Kuhusu kongani ya viwanda, alisema ni muhimu kuwa na maeneo hayo kwenye mikoa mingine, ili malighafi zinazozalishwa ziweze kuchakatwa na hivyo kukuza uchumi na kilimo kwa wananchi vijijini.
Prof. Wangwe alisema kongani hizo zitapunguza uagizaji wa bidhaa nje hivyo kuvutia teknolojia za wawekezaji wa kimataifa kuja kujenga viwanda nchini.
Kuhusu EACLC, alisema ni kituo kizuri ambacho serikali inapaswa kujenga kingine kwenye kanda zingine za nchi, ili kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa.
URANI NAMTUMBO
Safari ya kuzindua miradi hiyo ilianzia wilayani Namtumbo, cha majaribio cha uchenjuaji madini ya urani, unakadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 1.2.
Mradi huo unatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 8,700 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, huku serikali ikinufaika na mapato ya takribani Dola za Marekani bilioni moja kupitia kodi, mirabaha na gawio kutokana na umiliki wake wa asilimia 20.
Rais Samia alisema mradi huo unaiweka Tanzania katika hatua muhimu ya safari yake ya kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, teknolojia na rasilimali za ndani.
Takwimu zinaonesha kwamba katika eneo la Mto Mkuju pekee, kuna hifadhi ya tani 60,000 ya madini hayo, jambo linaloliweka taifa katika rekodi nzuri ya umiliki wa rasilimali hii.
BANDARI YA KWALA, KONGANI YA VIWANDA
Baada ya kutoka Namtumbo, Alhamisi (Julai 31), Rais Samia alizindua bandari kavu ya Kwala na kongani ya viwanda, miradi inayotajwa kuzalisha zaidi ya ajira 200,000 na uwekezaji wa Dola bilioni tatu.
Aidha, Kongani ya Viwanda ya Kwala, itakapokamilika, itakuwa na uwezo wa kuchukua viwanda zaidi ya 200, kutoa ajira za moja kwa moja 50,000 na zisizo za moja kwa moja 150,000.
Katika eneo la Kwala lenye zaidi ya hekta 1,000, viwanda zaidi ya 200 vinatarajiwa kujengwa kwa uwekezaji wa Dola bilioni tatu, zitakazoweza kuingiza mauzo ya Dola bilioni sita na kuleta ajira 250,000 zisizo za moja kwa moja pamoja na 50,000 za moja kwa moja kwa vijana wa mkoa wa Pwani.
EACLC
Akizindua kituo hicho cha biashara, Rais Samia alisema kitakuwa jukwaa la kimkakati kwa ajili ya kuongeza thamani ya bidhaa, kutengeneza ajira na kukuza ushindani wa Tanzania katika biashara ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), uwekezaji wa kituo hicho umeingiza mtaji wa Sh. bilioni 282 na kutoa ajira zaidi ya 2,000 wakati wa ujenzi; na kwamba, sasa kitatengeneza ajira 65,000 zikiwamo za moja kwa moja 15,000 na zisizo za moja kwa moja 50,000.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED