Wananchi: 2025 hatutaki wabunge ‘bubu’ bungeni

By Waandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 04:49 PM Aug 03 2025
Wananchi
Picha Mtandao
Wananchi

WAKATI Bunge likitarajiwa kuvunjwa rasmi leo, baadhi ya wananchi wameweka masharti ya wawakilishi wao wajao wawe ni wenye uwezo wa kujenga hoja, kuzungumzia kwa kina matatizo yao, ili yatatuliwe na si kuwa na wabunge ‘bubu’ bungeni.

Kadhalika, wamesema wanataka wabunge wenye uwezo wa kufuatilia matumizi ya fedha za serikali kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayotolewa kila mwaka, ili kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma.

Hati ya kuvunjwa kwa Bunge ilitolewa Julai 30, mwaka huu, ikiwa ni utekelezaji wa Ibara ya 92(2) ya Katiba ya Tanzania, inayompa Rais mamlaka ya kulivunja.

Katika hati hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan, alitangaza kulivunja rasmi Bunge Agosti 3, ili kutoa nafasi ya uteuzi wa wagombea.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Nipashe wananchi hao, walisema katika Bunge lijalo wanahitaji kupata wawakilishi walio na maono, ili kuwakilishwa vyema bungeni na kutatuliwa changamoto zao.

Mkazi wa Buchosa, Martine Mussa alisema awamu hii wanahitaji kupata wabunge watakao wawakilisha bungeni kwa kutoa hoja na mawazo yao, ikiwamo maboresho ya miundombinu ya barabara, afya, maji na elimu na si wanaoingia bungeni kwa ajili ya kukamilisha mikakati yao binafsi.

Alisema kumekuwapo mazoea katika kipindi cha kampeni wagombea ubunge  kuja na ahadi nyingi, lakini wakipewa uwakilishi wanasahau waliyoahidi.

“Kumekuwa na desturi ya viongozi hao kutokuwa na maono na taswira mpya katika maeneo yao, kwani mtu hana jipya analowaza kwa sasa, tunataka kuona kitu kipya kinaanzishwa pamoja na mawazo chanya kwenye uongozi, ili tubaki na alama ya uongozi wa mhusika,” Mussa.

Mkazi wa Miembeni mkoani Kagera, Mlokozi Mwombeki, alisema mategemeo makubwa ya wananchi kwa wabunge ni utendaji wa kazi ambao unawasaidia wanajamii kuondoa matatizo na kuwapa furaha ya kimaendeleo.

"Mbunge akiwa bungeni anasahau kwamba yeye ndiye mwakilishi wa matatizo ya wananchi,” alisema. 

Mwombeki alisema baadhi ya wawakilishi wa wananchi bungeni wamekuwa badala ya kuwakilisha wananchi, hubaki kuwa watetezi wa serikali tofauti na kile walichokiomba kwa wananchi, hivyo kuahidi kuwa kwa kipindi hiki wanahitaji kufanya uamuzi sahihi.

Mkazi wa Matopeni, Kata Kashai, Bernard Claveri, alisema hitaji la wananchi ni maendeleo na Bunge ndio linatunga sheria za kusaidia kuboresha maisha ya kila Mtanzania, hivyo hali ya wabunge kutokuhudhuria vikao na kushindwa kutoa hoja za kuwatetea ni kwenda kinyume na matakwa.

"Wakiwa wanatafuta kura utasikia ahadi nyingi sana, lakini akifika bungeni utetezi wa yale mambo hauonekani, miaka inaisha na kusonga mbele huku hakuna maendeleo. Ukiangalia kijiji na mtaa hakuna mabadiliko. Hatuwataki tena wa namna hii,” alisema Claveri.

Alisema wabunge wawatakao ni wale watakaosimamia hoja zinazotolewa wakati wa kampeni, kwani zitasaidia kumaliza tatizo la ajira na kusaidia katika uwezeshaji kwa wananchi na kuwafanya wawe na shughuli za kuwaingizia kipato.

Mkazi Hamgembe, Mogarn Jovina, alisema wanahitaji Bunge liwe kama la miaka 10 au 15 iliyopita,  ambalo wabunge wake walijenga hoja zinazogusa mwananchi na kutetea matatizo yao.

RIPOTI YA CAG IHESHIMIWE

Kadhalika, wananchi wamewataka wabunge watakaochaguliwa Oktoba 29, mwaka huu, wahakikishe wanafuatilia matumizi ya fedha za serikali kupitia ripoti ya CAG inayotolewa kila mwaka, ili kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma.

Mkazi wa Majengo Jimbo la Kahama, Daudi Jacob, alisema ni wabunge wachache walioweza kuzungumzia changamoto zilizoko kwenye majimbo yao, huku wakikaa kimya kuhusu hatua za kuchukua wanaosababisha upotevu wa fedha unaobainika kupitia ripoti ya CAG.

Aidha, alisema licha ya wabunge kuwa wawakilishi, lakini unapofika wakati wa ripoti hiyo, amedai wananchi hawapewi mrejesho kuhusu kinachofanyika, hivyo wanahujumu mali za umma.

 Mkazi wa Zongomela Kahama, Sakina Juma, alisema Bunge lijalo angependa kuona wabunge wenye uwezo wa kuwakilisha wananchi kutoka kwenye eneo lake, ili kusaidia kuboresha mazingira ya wananchi kiuchumi.

Mkazi wa Nyamilangano, Sebastian Lucas, alisema kwa sasa hawawataki wabunge wanaokwenda kukaa kimya, kwa kuwa wamebaini watu wa namna hiyo ni kama huingia bungeni kwa maslahi yao binafsi.

KURUDI JIMBONI

Mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, Alphat Athuman, aliweka wazi kuwa mbunge wanayemtaka ni atakayesimamia maslahi ya wananchi badala ya kujinufaisha binafsi.

Aidha, alisema wanataka mwakilishi ambaye kila mara atarudi kwao kufanya mikutano na kusikiliza kero zao na kuzisemea bungeni ili serikali izitatue.

"Hatutaki mwakilishi ‘bubu’ bungeni asiyeweza kuyasemea matatizo ya wananchi,” alisema Athumani.

MCHAMBUZI ANENA

Mchambuzi wa siasa nchini, Hamduny Marcel, akizungumza na Nipashe alisema kuna tofauti ya kutoa michango bungeni na kusaidia kuwaletea maendeleo wananchi wa jimboni lake.

Anasema kuzungumza ni talanta au kipawa cha mtu, akifafanua hoja yake kwamba, wapo wanaozunguza sana bila hoja za msingi na wanaozungumza kidogo, lakini kwa vitendo na wajenzi wa hoja zenye matokeo chanya kwa wananchi na katika wizara husika.

Marcel anasema wabunge wanaopewa ridhaa wanalo jukumu la kuzungumza kwa vitendo na kuhakikisha yanapatikana majawabu yanayowagusa wananchi katika majimbo wanayotoka.

Imeandaliwa na Marco Maduhu (SHINYANGA), Elizabeth Seleman (BUCHOSA), Restuta Damian (KAGERA), Shaban Njia, (KAHAMA), Remmy Moka na Vitus Audax (MWANZA)