Zitto: Tumetathmini kumteua Mpina kuwania urais

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 05:35 PM Aug 10 2025
Zitto Kabwe
Picha: Mtandao
Zitto Kabwe

CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimesema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, vijana wanakwenda kuking'oa Chama Cha Mapinduzi (CCM), madarakani.

Kauli hiyo imetolewa leo na Kiongozi mstaafu wa Chama hicho, Zitto Kabwe, wakati akizungumza visiwani Zanzibar kwenye tukio la kuwatambulisha wagombea wa urais wa chama hicho.

Zitto amesema mgombea urais wa chama hicho kwa Jamhuri, Luhaga Mpina pamoja na mgombea urais Zanzibar, Masoud Othman Masoud, wataongoza mapambamo ya kuing'oa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

"Mpina ni mmoja ya wanasiasa ambao akikwambia nyeupe ni nyeupe, akikwambia ni nyeusi ni nyeusi.

"Ninaelewa wasiwasi wenu wa huko tulikotoka. Viongozi wenu wanaelewa na wamefanya tathmini ya kutosha, sisi viongozi tunamchukulia Mpina thamani, kwa sababu tunamwamini," amesema Zitto.

Amesema historia ya Mpina inaonesha ni mwanasiasa mwenye msimamo.

"Mpina ni mwanasiasa mwenye msimamo, ni mwanasiasa anayetaka kuona mabadiliko katika nchi, ameamua kuungana wenzake, kutekeleza wajibu muhimu, ni kijana ambaye amekubaliana na kuungana na vijana wenzake kuiongoza vita ya wajibu wa kizazi ya kwenda kuing'oa CCM madarakani. 

"Chama chenu kimewaletea mgombea ambaye tuna hakika kwa umri wake na nguvu alizonazo, hekima yake na kwa kushirikiana na mgombea mwenza mwenye uzoefu wa siasa, vijana tutafanya mabadiliko ya nchi hii."

 "Tumefanya tathmini, tumetizama historia ya nyuma, makoa ya nyuma na tumeyarekebisha, tuko vizuri, tutafaya vizuri msiwe na mashaka. Hiki chama ni chama ambacho kina radhi ya Maalim Self Sharif Hamad (hayati), hakiwezi kuwa chama kinachofanya maigizo katika siasa."