WANANCHI wa Kijiji cha Terrat, wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wamesema wanajivunia uwapo wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tukuta na kuueleza mradi huo kuwa mkombozi kwa watoto wa kike katika eneo hilo.
Akizungumza Agosti 23, 2025, baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Terrat, Kone Medukenya, amesema shule hiyo italeta mapinduzi makubwa ya elimu kwa watoto wa kike ambao kwa muda mrefu walikosa fursa za kusoma kutokana na changamoto ya umbali na miundombinu duni.
Medukenya ameeleza kuwa shule hiyo itakuwa na vyumba vya madarasa 12, maabara nne za sayansi, mabweni sita, nyumba 16 za walimu, jengo la utawala, chumba cha kompyuta na seva, pamoja na miundombinu mingine ikiwamo bwalo la chakula, jiko, ukumbi, kisima kirefu cha maji na uzio wa shule.
Ujenzi wa shule hiyo unatekelezwa na Shirika la ECLAT Development Foundation Tanzania, kwa ufadhili wa Shirika la Upendo Foundation kutoka Ujerumani, kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 4.6, ikiwamo Sh milioni 216 thamani ya ardhi iliyotolewa na kijiji hicho.
Prof. Mkenda ameeleza kuwa shule hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kushirikiana na wadau wa maendeleo kuboresha miundombinu ya elimu nchini na kusisitiza kuwa ifikapo mwaka 2027, kila mtoto atatakiwa kusoma hadi kufikia kidato cha nne, ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa elimu ya lazima kwa miaka 10.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED