NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ametoa rai kwa wanamichezo kufanya uchunguzi wa afya zao, kwa kuhusisha vipimo vyote muhimu vya mwili.
Amesema wazingatie vipimo vya vya moyo, damu na viungo vyote vya mwili, ili kujihakikisha usalama wa afya zao.
Ameliomba Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI), kuendelea kushirikiana na taasisi za afya nchini na kuweka mfumo sahihi wa upimaji kwa wanamichezo.
Dk. Biteko ametoa rai hiyo leo, Septemba 7, 2025 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati akifungua rasmi mashindano ya 39 ya SHIMIWI yaliyotanguliwa na maandamano ya watumishi wa umma.
Ametaja masuala mengine muhimu ya kuzingatiwa kwa wanamichezo ikiwamo mazoezi ya awali na mbinu nyingine mbalimbali kwa kujenga uimara wa mwili.
Ameongeza kwa kusema: “Nimejulishwa kwamba, katika michezo ya mwaka wa jana mlisajili watumishi 2,995. Na mwaka huu 2025 mmesajili watumishi 3,353 kushiriki michezo hii, ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 12 hongereni sana.”
Pia, ameipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na viongozi wa SHIMIWI, kwa kazi ya kuratibu, kusimamia na kuendeleza michezo nchini.
Dk. Biteko pia amewataka waajiri kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hssan, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watumishi wanaoshiriki SHIMIWI.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa, tasnia ya burudani Tanzania, ambayo michezo ipo ndani yake imeendelea kukua kwa kasi na kuchangia sehemu muhimu katika Pato la Taifa na kuongeza ajira nchini.
Ametolea mfano kwa mwaka 2022/2023 sekta hiyo imekua kwa asilimia 15 na mwaka 2023/24 kwa asilimia 18.
Aidha, uwapo wa watumishi wanaoshiriki SHIMIWI zaidi ya 3,000 jijini Mwanza, umesaidia kutengeneza ajira na kuchangia mzunguko wa fedha.
“Nawaomba viongozi muweke mikakati ya kuhakikisha manufaa haya yanawagusa watanzania wa maeneo yote nchini kwa maslahi mapana ya taifa kwa ujumla,” amesisitiza Dk. Biteko.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema shughuli za kampeni mkoani humo, zinaendelea vizuri na Oktoba 29, 2025, wananchi watajitokeza kwa wingi kupiga kura.
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema:
“Wizara yetu itaendelea kuhakikisha michezo hii inafanyika kwa haki, sisi kama wizara tunamshukuru Rais kwa maelekezo yake na kutoa raslimali fedha, ili kukuza sekta ya michezo nchini,” amesema Msigwa.
Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba, amesema Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Baraza la Michezo la Taifa, imefanya shughuli zake kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuleta matokeo chanya.
Mashindano ya Michezo ya 39 ya SHIMIWI kwa mwaka 2025, yanayoongozwa na kaulimbiu ‘Michezo kwa Watumishi Huongeza Tija Kazini, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 29 Oktoba 2025 kwa Amani na Utulivu Kazi Iendelee’, yatafikia tamati Septemba 16, 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED