SULUHU iliyoipata juzi timu ya JKT Tanzania ikiwa ugenini, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi dhidi ya Namungo FC, imeifanya timu hiyo kucheza mechi tatu bila kufunga bao wala kupata ushindi kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mara ya mwisho JKT Tanzania kupata ushindi na kufunga bao ilikuwa ni, Novemba 29, mwaka huu, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara, ilipoifunga Fountain Gate bao 1-0, lakini baada ya hapo imetoka suluhu mechi tatu mfululizo.
Ilifanya hivyo dhidi ya Pamba Jiji, Desemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam na Mashujaa FC kwenye uwanja huo huo, Desemba 15, mwaka huu, kabla ya juzi kupata tena suluhu dhidi ya Namungo.
Suluhu hiyo inaifanya timu hiyo kufikisha pointi 19 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa kwenye nafasi ya nane, ikicheza michezo 14, ikisalia mchezo mmoja tu kumaliza mzunguko wa kwanza.
Namungo imemaliza mechi zake 15 za mzunguko wa kwanza ikiwa kwenye nafasi ya 12, ikikusanya pointi 14 mpaka sasa.
Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amewasifu wachezaji wake kwa kupambana kuipata pointi moja, akisema lilikuwa ni lengo lao la pili kama wakikosa zote tatu.
"Niwapongeze vijana wangu, mechi kucheza ugenini si rahisi, tulikuja hapa kwa malengo mawili, tupate pointi tatu na kama tukishindwa basi moja, na tumeipata.
"Tumetengeneza nafasi mbili hatukuzitumia na tumecheza na timu bora, niipongeze Namungo wamecheza vizuri," alisema.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, alionekana kuridhika na matokeo hayo kutokana na timu aliyocheza nayo, akisema ni moja kati ya vikosi bora kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa.
"Matokeo nimeyapokea vizuri tu kwa sababu nimetoka suluhu na moja kati ya timu nzuri tu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
"JKT Tanzania ni timu nzuri sana, inacheza kitimu na ina wachezaji wazuri, nimeridhika na matokeo, sasa tunakwenda kujipanga na mechi za mzunguko wa pili," alisema Mgunda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED