WAKATI kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' kikitarajia kurejea kesho kutoka Misri kwa ajili ya kushiriki mashindano ya CECAFA, kocha wa timu hiyo, Hemed Morocco, amelalamikia kuwapo kwa mashindano hayo.
Morocco, amesema mashindano hayo ya CECAFA hayajaja wakati mwafaka kutokana na kuingiliana na maandalizi yao kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Kocha huyo ameonesha wasiwasi kuwa wachezaji wanaweza kuwa na fatiki kuelekea mchezo wa ufunguzi wa CHAN dhidi ya Burkina Faso, Agosti 2, kwani watakuwa wamecheza michezo kadhaa ya michuano hiyo ya CECAFA siku chache kabla ya ufunguzi wa fainali za CHAN.
Michuano hiyo ya CECAFA 4 Nations, inatarajiwa kuanza kupigwa Jumatatu ijayo hadi Julai 27, ikizishirikisha nchi ambazo ni wenyeji wa CHAN, Tanzania, Kenya na Uganda, pamoja na timu waalikwa, Congo Brazaville, lengo likiwa kuzipa mazoezi kabla ya fainali hizo.
"Ni michuano mizuri lakini haikuja kwenye wakati sahihi, kwangu mimi nadhani ingekuja wiki mbili zilizopita ingekuwa vyema sana ili kutuweka sawa kuelekea CHAN, lakini tutacheza mechi tatu ndani ya siku tano au sita, halafu tunakwenda kucheza mchezo mgumu, Agosti 2, tutakuwa na ugumu fulani hasa kwenye fatiki," alisema Morocco na kuongeza,
"Kwa sababu hata hizo mechi za CHAN zitakuwa zinachezwa kwa mfuatano, baada ya siku tatu au nne, itawachosha sana wachezaji, binafsi naona ratiba imetubana sana, lakini hatuna jinsi itabidi tucheze, tutaangalia tutafanyaje ili tusiwachoshe wachezaji," alisema Morocco.
Ratiba inaonesha, Stars itacheza dhidi ya Congo Brazaville, Jumatatu, kwenye Uwanja wa Tanzanite, Babati, kabla ya kurejea tena dimbani, Julai 24, kucheza dhidi ya Kenya na mwisho kumalizia mechi yake ya mwisho dhidi ya Uganda, Julai 27.
Stars itabidi iondoke mjini Ismailia ilipokuwa imepiga kambi, ambapo kwa mujibu wa kocha Morocco, wachezaji wake wameimarika.
"Tayari wana utimamu wa mwili, unaona kabisa sasa wana nguvu, wanakimbia, wana ari, inatia moyo, kambi hii ilikuwa kambi bora sana," alisema.
Jumla ya timu 19 zitashiriki fainali za CHAN, Stars ikiwa Kundi B na timu za Burkina Faso, Afrika ya Kati, Madagascar, na Mauritania.
Kundi A, lina timu za Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Morocco na Zambia, huku Kundi C, likiundwa na timu za Algeria, Guinea, Niger, Afrika Kusini na Uganda.
Timu za Congo Brazaville, Nigeria, Senegal na Sudan, zinaunda Kundi D.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED