MABAO matano yaliyofungwa na Shomari Kapombe, Jean Ahoua, Fabrice Ngoma na Steven Mukwala aliyepachika mawili, jana yaliirejesha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kupata ushindi wa 5-2 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo mkali wa aina yake uliochezwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.
Simba imekuwa ikihangaika kupata ushindi kwenye uwanja huo kwa misimu mitatu sasa ambapo ilikuwa ikiambulia sare na kichapo.
Ushindi huo umeifanya kuongoza ligi, ikifikisha jumla ya pointi 34, mabao 29 ya kufunga, kuruhusu matano nyavuni mwake hadi sasa ikiwa imecheza mechi 13.
Unakuwa ni ushindi mkubwa zaidi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, kwani hakuna timu yoyote iliyowahi kupata idadi hiyo ya mabao kabla.
Mechi hiyo pia imeweka rekodi ya kuwa na mabao mengi zaidi kwenye ligi mpaka sasa, kutokana na kuzaliwa mabao saba kwenye mchezo mmoja.
Moja ya tukio ambalo wanachama na mashabiki wa Simba walifurahia ni kumuona kiungo mshambuliaji wao mpya, Elie Mpanzu, akiichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza, kama walivyotarajia alikuwa kwenye kiwango kikubwa ambacho kilichangia ushindi huo.Shomari Kapombe ndiye alianza kufungua kitabu cha mabao dakika ya 12 ya mchezo, alipounganisha krosi iliyopigwa na Mohamed Hussein, 'Tshabalala'.
Mpira ulianzia kwa Ahoua, ambaye aliupeleka pembeni upande wa kushoto, beki huyo akiwa amepanda mbele alimimina krosi ambayo Steven Mukwala aliruka juu na kuukosa mpira, lakini Kapombe alikuwa kwenye eneo zuri akaukwamisha wavuni.
Ni bao la pili kwa beki huyo wa kulia wa Simba msimu huu, huku Tshabalala naye akifikisha 'asisti' ya tatu.
Alikuwa ni Ahoua, aliyeiandikia Simba bao la pili kwa mkwaju wa faulo dakika moja kabla ya mapumziko, baada ya yeye mwenyewe kuchezewa madhambi na Abdallah Mfuko, nje kidogo ya eneo la hatari.
Kiungo mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast, aliupitisha mpira juu ya vichwa vya wachezaji na kugonga mwamba wa juu, ukadundia ndani na kurudi uwanjani, huku mwamuzi Tatu Malongo akiita kati baada ya kupata ishara kwa msaidizi wake kuwa ulikuwa umevuka mstari.
Linakuwa bao la sita kwa mchezaji huyo msimu huu, akiwa ndiye anaongoza kwa ufungaji mabao katika kikosi hicho.
Dakika ya 40, kiungo mshambuliaji wa Simba, Awesu Awesu alilazimika kutoka nje kutokana na kuumia na nafasi yake ilichukuliwa na Ladack Chasambi, ambaye alitoa 'asisti' tatu, mbili kwa straika wa Uganda, Mukwala na moja kwa Fabrice Ngoma.
Kiungo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Ngoma, aliipatia Simba bao la tatu dakika ya 53 kwa kichwa, akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Chasambi.
Kona hiyo ilitokana na Debora Fernandes kupiga shuti kali karibu na eneo la hatari ambalo lilimbabatiza Mohamed Mussa na kuwa kona.
Mukwala alipachika bao la nne, dakika ya 66 baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Chasambi, kuwatoka mabeki wa Kagera Sugar na kumwekea mfungaji kwenye nafasi nzuri, ambapo alitisha kama anapiga na mguu wa kulia, hali iliyosababisha Mfuko na kipa wake Ramadhani Chalamanda kupoteana na kumpa nafasi mfungaji kumalizia kwa mguu wa kushoto.
Ilionekana kama Simba na Kocha Fadlu Davids na wachezaji wake waliridhika na mabao hayo, wakafanya mabadiliko ambayo yaliyonekana kuwaathiri na kuruhusu mabao mawili dakika za mwishoni mwa mchezo.
Walioingia ni Joshua Mutale, Kelvin Kijili, Yusuph Kagoma, badala ya Mpanzu, Ngoma na Mavambo.
Mabadiliko hayo yalionekana kuwafanya wenyeji kupata uhai na kulishambulia kama nyuki lango la wapinzani wao.
Alikuwa ni Datius Peter aliyeipatia Kagera Sugar bao la kwanza dakika ya 79, akionekana kusahaliwa na mabeki wa Simba, akaingia ndani ya eneo la hatari na kuukwamisha wavuni.
Mukwala alifunga bao la tano dakika tano kabla ya mchezo kumalizika, akimalizia kazi kubwa iliyofanywa na Chasambi kwa mara nyingine.
Straika huyo anatimiza bao la nne kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, ukiwa ni msimu wake wa kwanza akiwa amesajiliwa kutoka Asante Kotoko ya Ghana.
Dakika za majeruhi, Cleophace Mkandala alipiga shuti kali la mbali ambalo lilikwenda moja kwa moja hadi wavuni na kumuacha kipa Moussa Camara akiruka bila mafanikio, likiwa ni bao la pili la Kagera Sugar katika mchezo huo.
Simba ilianza mpira kwa kasi na sekunde ya 32 tu tayari walikuwa wamefika kwenye lango la wenyeji wao kwa kugongeana, mpira ulimfikia, Jean Ahoua aliyepiga shuti la mbali mpira ulionekana kama unataka kutinga wavuni, lakini ukatoka juu kidogo ya lango.
Kagera Sugar ilijibu shambulio hilo dakika ya nne, pale walipowanyang'anya mpira wachezaji wa Simba waliokuwa wameanzia nyuma, pasi ya mwisho ilifika kwa Geofrey Manyasi ambaye shuti lake lilitoka pembeni kidogo ya lango.
Dakika ya sita, nusura Debora Fernandes aipatia Simba bao, baada ya shuti lake lililoonekana kwenda wavuni kumgonga David Luhende na kurejea uwanjani kabla ya kuokolewa.
Shambulizi hilo lilifanywa na Mpanzu aliyekuwa akicheza mechi ya kwanza akiwa na timu hiyo, akishirikiana na Kapombe.
Kipigo hicho kinaiacha Kagera Sugar katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 11, na ikiwa imemaliza michezo yake ya mzunguko wa kwanza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED