KOCHA Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema wanachohitaji kwenye mchezo wa leo ni pointi tatu tu na hakuna kingine, kwani ndicho kinachosubiriwa na wanachama na mashabiki wa timu yake ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuelekea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Yanga leo inashuka tena kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, kucheza dhidi ya Maafande wa Prisons, timu ambayo haijashinda mchezo wowote kati ya minne iliyocheza mfululizo.
Kocha huyo raia wa Ujerumani, amesema wala hawatoidharau Prisons kutokana na matokeo yake mabaya kwenye Ligi Kuu, au nafasi iliyonayo kwa sasa, badala yake wataingia uwanjani wakiwa na malengo yao ya kupata ushindi ili kujiwekea mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa ambao anasema vita inaonekana kuwa kubwa kileleni.
"Maandalizi tayari, itakuwa mechi ngumu, tunacheza na timu inayokabia chini na kushambulia kwa kushtukiza, inatakiwa tuwe makini ili kushinda mechi hii, tutafanya kila linalowezekana kushinda mechi hii kwani tunahitaji pointi tatu.
"Hatuwezi kuidharau Prisons kwa sababu ya matokeo yake mabaya, tunatakiwa kuiheshimu kila timu, mpira wa miguu ni mchezo wa ajabu sana ambao mwisho wa siku unaweza kuumiza moyo wako kwa sababu ya dharau," alisema kocha huyo.
Yanga itacheza mchezo wa 13 leo, ikiwa na pointi 30, na kama ikishinda itafikisha pointi 33 ambazo kwa sasa inazo Azam FC ambayo imeshamaliza mechi zake za mzunguko wa kwanza.
Kabla ya mchezo wa leo, Yanga imecheza michezo 12, ikishinda 10, ikipoteza miwili, haijatoka sare hata moja, ina mabao 19, ikiruhusu sita nyavuni kwake.
Kwa upande wa Prisons, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Shaaban Mtupa, alisema alikuwa na kazi kubwa ya kuwarudisha kwenye morali wachezaji wake ambao walionekana kama wamekata tamaa kutokana na matokeo mabaya ya siku za hivi karibuni.
Hata hivyo, alisema kazi yake imezaa matunda kwani wachezaji wa Prisons sasa wamemka na wako tayari kwa mchezo huo.
"Kazi ya kwanza niliyoifanya kubwa ni kurudisha ari ya wachezaji ambao inaonekana kabisa ilikuwa chini, kingine ni kuwafanya wajiamini, hivi vipindi vya mpito hata sisi wakati tunacheza mpira tumevipitia.
"Kwa sasa naona wameamka na wapo tayari kwa mchezo wa kesho. Ni muhimu sana kwetu kwa sababu hatujapata matokeo mazuri mechi kadhaa nyuma, lakini sasa tunahangaika kupata matokeo ya ushindi," alisema straika wa zamani wa timu hiyo.
Hata hivyo alikiri haitokuwa mechi rahisi kutokana na ubora wa timu ambayo wanakwenda kukutana nayo.
" Tunakwenda kucheza na Yanga ambayo ni timu nzuri sana na wachezaji wanaoweza kuamua matokeo muda wowote, lakini na sisi tumeyafanyia kazi, tunataka kutumia udhaifu waliokuwa nao kuwaadhibu ili kupata ushindi," alisema.
Kwa sasa Prisons inakamata nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 11 kwa michezo 14 iliyocheza.
Mara ya mwisho kupata ushindi ilikuwa Novemba 3, mwaka huu, Uwanja wa Sokoine Mbeya, iliposhinda bao 1-0 dhidi ya KenGold, baada ya hapo ilichapwa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania, mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union, suluhu dhidi ya Kagera Sugar na kuchapwa mabao 2-0 dhidi ya Singida Black Stars.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED