KLABU ya Simba imesema kwa mara ya kwanza baada ya misimu kadhaa, usajili wanaoufanya kuelekea msimu ujao ni mapendekezo ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids kwa asilimia 100, tofauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wakisajili bila kocha.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema usajili wa safari hii unasimamiwa na kocha Fadlu, huku akikiri kuwa jambo hili linafanywa kwa mara ya kwanza baada ya misimu kadhaa, kwani mara nyingi wamekuwa hawana kocha wanapomaliza ligi, hivyo kuwa na kazi ya kusaka wachezaji na makocha.
Kumbukumbu inaonesha hata msimu uliopita, Simba ilisajili wachezaji zaidi ya 15, wakati huo huo ikampata kocha mpya, Fadlu ambaye alikuja na wasaidizi wake kuja kuchukua nafasi ya Juma Mgunda, ambaye alikaimu nafasi ya Abdelhak Benchikha, raia wa Algeria, aliyeondoka.
"Kwa miaka mingi, msimu huu kwa asilimia 100 tunafanya usajili kwa mapendekezo ya benchi la ufundi, hususani mwalimu, Fadlu Davids. Misimu kadhaa nyuma mara nyingi ilikuwa misimu kama hii inatukuta hatuna kocha," alisema Ahmed na kungezea,
"Ligi ilipoisha kocha alitoa mapendekezo yake, akawasilisha ripoti ambayo inataja jina la mchezaji na timu ambayo anaichezea. Lakini yapo maeneo ambayo hakuwasilisha majina, bali eneo lenye mapungufu na uwezo wa mchezaji anayemhitaji, kwa maana hiyo safari hii tunakwenda bega kwa bega na mapendekezo ya kocha Fadlu," alisema Ahmed.
Alisema kocha wao alipendekeza majina ya wachezaji wote wa ndani na nje ya nchi, na tayari wamewapata wachezaji wote wa ndani, na wanaedelea na usajili wa wachezaji wa nje.
"Fadlu ameridhishwa na mipango ya Simba na ameamua kuleta wanajeshi wake ili kuifanya kazi ipasavyo na sisi kama klabu hatujamuangusha, maeneo yote aliyopendekeza, wachezaji wote aliowahitaji tumefanikiwa kuwapata, wengine tupo kwenye hatua za mwisho kabisa kumalizana nao, hivi ninavyozungumza viongozi wetu wametapakaa nchi mbalimbali za Kiafrika kwa ajili ya kumalizana na wachezaji husika tuje kuwaleta kwenye kikosi chetu," alisema.
Alikumbusha kuwa bado hawajamaliza kutoa 'thank you' kwa wachezaji ambao hawatokuwa nao msimu ujao.
"Bado tunaendelea na 'thank you', hazijaisha Simba, nadhani zitakuwa zimebaki tatu kama si nne, baada ya hapo tutaanza kutambulisha wachezaji wapya, wale wanaodhani labda hatujasajili wanajidanganya," alisema.
Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa Bodi wa Wakurugenzi, Mohamed Dewji, amesema alikuwa na mazungumzo na kocha Fadlu kuhusu mustakabali wa klabu hiyo, kuelekea msimu ujao na kukubaliana kujenga kikosi.
"Nimefurahi kuwa na mazungumzo ya maana na Kocha Fadlu, katika msimu wake wa kwanza, akiwa na kikosi kipya na benchi jipya la ufundi, ameiongoza Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF.
Chini ya yake, Simba imefika fainali ya pili ya kimataifa katika historia ya klabu.
Msimu huu ulikuwa wa kujenga timu. Na bado tukafika fainali, licha ya upinzani mkali. Simba haitazulika msimu ujao," alisema Mo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED