KLABU ya Yanga imesema imebakisha mchezaji mmoja tu ili ikamilishe usajili wa nyota wapya kuelekea msimu ujao, huku ikitamka rasmi kuwa mwaka huu watapiga kambi nje ya nchi kujiandaa na msimu mpya wa mashindano.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema zoezi ya usajili kwa upande wao limekwenda vizuri ambapo kwa sasa wamebakisha mchezaji mmoja tu ili wafunge pazia la usajili.
"Tunafunga kazi usajili wiki hii, bado mchezaji mmoja tu, uzuri tumeshatoa taarifa ya kuanza kutangaza wale ambao tutawaacha, waliomaliza mikataba na wale ambao hatutotaka kuendelea nao, tutakuja kwa wachezaji tuliowaongezea mikataba na tutamalizia na wapya," alisema Kamwe.
Ofisa Habari huyo alisema klabu hiyo itaanza kazi hiyo, Jumapili ijayo na itamalizika, Agosti 3 mwaka huu.
Kamwe pia alisema safari hii kikosi chao kitapiga kambi nje ya nchi ambayo ataitangaza hapo baadaye.
"Kambi yetu itafanyika kwa awamu mbili, tutaanza ya ndani hapa kwenye wiki za kwanza, baada ya hapo tutakwenda Rwanda tukawape sapoti wenzetu Rayon Sports kwenye tamasha lao, baada ya hapo tutakuwa na awamu ya pili ya 'pre season', ambayo hii tutaifanya nje ya mipaka ya Tanzania, hii ndiyo plani ambayo tuko nayo mpaka sasa," alisema.
Yanga majuzi ilitangaza kuwa itakuwa na mchezo maalum wa kirafiki dhidi ya Rayon Sports, utakaofanyika, Uwanja wa Amahoro, Kigali, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya tamasha la klabu hiyo la 'Rayon Sports Day'
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED