4,109 wachukua fomu kuwania ubunge bara, visiwani

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 01:44 PM Jul 03 2025
news
Picha Mtandao
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema waliochukua fomu kuomba ridhaa ya ubunge kupitia majimbo Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar ni wanachama 4,109.

Amesema kati yao waliochukua Bara ni wanachama 3,585 na Visiwani Zanzibar ni 524.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, ameyasema hayo leo Julai 3, 2025 wakati akitoa taarifa ya mchakato wa CCM wa uchukuaji fomu uliofanyika kwa siku tano kuanzia Juni 28, 2025 na kuhitimishwa Julai 2, 2025.

“Chama Cha Mapinduzi kimefurahishwa na hamasa kubwa iliyojitokeza katika mchakato huu. Ninyi ni mashahidi uchukuaji wa fomu CCM safari hii umevunja rekodi, habari ya mjini ni uchukuaji fomu CCM.

“Hii inaonesha CCM kinaaminika kwa Watanzania na ni chama imara, kina sera nzuri na ndio matumaini ya Watanzania. “Tumeona makundi mbalimbali yamechukua fomu, vijana, wanawake, watu wa kila rika wamechukua fomu,” amesema.

Makalla amesema kwa takwimu waliochukua fomu kwenye majimbo 272 ya Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar, jumla yao ni 4,109.

Makalla amesema kwa upande wa uwakilishi Zanzibar waliochukua fomu ni wanachama 503 na UWT ni 623 Bara na ndani yake yako 91 makundi maalum na Zanzibar wamechukua wanane na viti maalum uwakilishi ni tisa, ambapo jumla yao ni 640.

Amesema waliochukua fomu kupitia UVCCM ni wanachama 161, kati yao Bara ni 154 na Zanzibar wako saba.

"Jumuiya ya Wazazi waliochukua jumla ni 62 kati yao, Bara ni 55, Zanzibar ubunge viti maalum ni watatu na uwakilishi ni wanne.

Makalla amesema hadi wanahitimiza mchakato huo kwa ubunge na uwakilishi waliochukua fomu kuonesha nia ni 5,475. Kwenye nafasi za udiwani wanaendelea kuchakata taarifa zake katika kata zote 3,660, hivyo tunaweza kuwa na wagombea 15,000. Kwa hiyo, kwa CCM waliojitokeza kuchukua fomu nafasi udiwani, ubunge tunaweza kuwa na na jumla wote wanaweza kufikia 20,000.

"Idadi ya wanawake majimboni waliochukua fomu ni 263, "amesema