Bawasiri; ugonjwa wenye unasaba na faraghani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:02 PM Jul 03 2025
Faragha ya vyoo katika mifumo tofauti
Picha: MTANDAO
Faragha ya vyoo katika mifumo tofauti

KUNA ungojwa unaoitwa Bawasiri, ambao haujulikani kwa kundi kubwa la jamii. Unahusu kuvimba mishipa ya damu iliyopo ndani au katika eneo linalozunguka njia ya haja kubwa.

Ni hali inayoweza kusababisha nyama kujitokeza nje. Hivyo, bawasiri, inaweza kuwa ya ndani au nje na unasababisha muwasho, maumivu na damu au hali ya kamasi kutoka wakati mtu anajisaidia haja kubwa, ingawa kuna wakati hauna dalili. 

Madhara ya bawasiri ya ndani ni pamoja na damu kutoka wakati wa kujisaidia, pia damu kuganda ndani ya mishipa ya damu na maumivu.

Kutokea bawasiri, kuna wakati huhusishwa na hali kama uzee, ujauzito, kuharisha au choo kufunga (constipation).

Pia, kuna maradhi ya saratani kwenye nyonga au kuketi kwa muda mrefu. Tiba yake, hutegemea ni bawasiri aina husika na ukubwa wa tatizo, matibabu yakihusisha matumizi ya dawa au upasuaji mdogo.

DALILI ZILIVYO

Inakadiriwa asilimia 40 ya watu wenye bawasiri, hawana dalili za moja kwa ambazo ni: maumivu, mwasho na hisia ya kitu kinachokera katika eneo linalozunguka njia ya haja kubwa. 

Baadhi ya watu hupata shida kujisaidia haja kubwa na wanatokwa na damu wanapojisaidia na kuna wakati mishipa ya damu huweza kujitokeza nje. Hali hiyo inapotokea, inatajwa anaweza mtu akahisi uvimbe mdogo katika eneo husika.

Inatajwa, ugonjwa Bawasiri hutokea pale shinikizo linaongezeka kwenye mishipa ya damu inayozunguka njia ya haja kubwa, ikiwa ni matokeo ya kitu kinachokandamiza utumbo, kama vile wakati wa ujauzito.

Ni hali inayotokea kwa mtu anapojikamua sana wakati wa kujisaidia haja kubwa, kutokana na kufunga choo au kuharisha kwa muda mrefu. 

Hali hiyo hutokea sana na hutokea zaidi kadri umri unavyoongezeka. Watu wenye uzito unaopita kiasi, nao wana uwezekano mkubwa wa kupata bawasiri. 

Wataalamu wa afua ya kundi hilo wana orodha zaidi ya vingine vinavyoongeza hatari ya kupata bawasiri ni pamoja na:

•            Uzito wa mwili kupita kiasi, ujauzito, kula vyakula visivyo na nyuzi (fibre) za kutosha

•            Kubeba vitu vizito kila mara.

•            Kuhara kwa muda mrefu na kufunga choo 

•            Kujamiiana kinyume na maumbile.

•            Historia ya uwepo ugonjwa wa bawasiri katika familia

•            Magonjwa yanayoathiri njia ya haja kubwa

•            Kuketi kwa muda mrefu

•            Uzee na matatizo ya kutopata choo.

UTAMBUZI NA TIBA

Bawasiri inatambuliwa kuanzia maelezo ya mgonjwa kwa daktari, pia kuchunguzwa njia ya haja kubwa. 

Uchunguzi huo wa njia ya haja kubwa hujumuisha kuangalia eneo hilo na kuingiza kidole taratibu kuchunguza sehemu ya ndani ya njia ya haja kubwa. 

Ikiwa bawasiri hazionekani kirahisi, au sababu ya kutoka damu haijaeleweka vizuri, uchunguzi wa ziada hufanywa kupata ukweli wa kina wa dalili hizo.

Matibabu: Bawasiri inatibika na kuna njia mbalimbali za kutibu bawasiri. Tiba halisi inanazia kuhakikisha mhusika anapata choo laini na kuepuka kufunga choo, ili kuepuka hali mbaya zaidi. 

Pia, kuna dawa za kupaka kwa kuingiza katika njia ya haja kubwa (suppositories) zikisaidia kupunguza uvimbe, mwasho na maumivu.

Kuna matibabu mengine ambapo sindano au kamba maalum hutumika ili kupunguza ukubwa wa mishipa ya damu. Dawa ya ‘Bawasiri sugu’ huwa ni upasuaji.

KINGA YAKE

Kuhakikisha unapata choo laini kunasaidia kuzuia bawasiri na kupunguza kujirudia kwa dalili zake. 

Hiyo inawezekana kwa kula vyakula vyenye nyuzi (fibber), kunywa maji ya kutosha, kuwa na uzito unaofaa, kuepuka kukaa kwa muda mrefu, kuepuka kujikamua wakati wa haja kubwa na kuepuka kubeba vitu vizito kila mara. 

HALI YA JUMLA

Bawasiri ni hali inayoweza kukera, lakini mara nyingi hazina madhara makubwa kwa afya ya binadamu na unaweza kuisha wenyewe ndani ya wiki. 

Bawasiri mara nyingi hujirudia, na hali huzidi kuwa mbaya kadri muda unavyosonga mbele.

Hutajwa kuwa tatizo la kawaida, ila linaweza kuathiri watu wengi wakati fulani maishani mwao. 

Kwa bahati nzuri, kuna hatua ambazo mtu anaweza kuchukua kuboresha hali hii au kuzuia kujirudia. Kwa mfano, kuhakikisha ulaji wa chakula chenye nyuzi (fibber) na kunywa maji ya kutosha kunaweza kusaidia kuzuia tatizo la bawasiri.

Ili kupunguza dalili za Bawasiri, mtu anaweza kujaribu matibabu ya nyumbani kama vile kujikanda kwa barafu ili kupunguza uvimbe au kutumia dawa za kupunguza maumivu. 

Hata hivyo, ni muhimu kushauriana na daktari ikiwa dalili zinazidi kuwa mbaya au nafuu haijapatiakana baada ya muda mfupi ili kupata ushauri na matibabu sahihi.