REA yasambaza mitungi, majiko ya gesi kwa watumishi 461 Magereza Mara

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:48 PM Jul 02 2025
REA yasambaza mitungi, majiko ya gesi kwa watumishi 461 Magereza Mara
Picha: Mpigapicha Wetu
REA yasambaza mitungi, majiko ya gesi kwa watumishi 461 Magereza Mara

Katika kuendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imegawa jumla ya mitungi ya gesi ya kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili 461 kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Mara.

Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa mitungi hiyo iliyoanza kugaiwa katika Gereza la Wilaya Musoma leo Julai 02, 2025, Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Lucas Malunde amesema kuwa mradi huo umelenga kuwafikia watumishi wa magereza 15,126 wote nchini.

Amesema kuwa, Wakala wa Nishati Vijijini uliingia makubaliano na Jeshi la Magereza Septemba 13, 2024 uliolenga kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Magereza yote nchini.

Mkataba huo wenye gharama ya Shilingi Bilioni 35.23 umelenga kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia, ujenzi wa miundombinu ya biogas, ujenzi wa miundombinu LPG, usambazaji wa mitungi ya gesi pamoja na majiko ya sahani mbili kwa watumishi wa magereza, usambazaji wa mkaa mbadala, ununuzi wa mashine za kutengenezea mkaa mbadala na kuwajengea uwezo watumishi wa magereza kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Serikali kupitia REA imeweza kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia na sasa Magereza yote Tanzania Bara yanatumia nishati safi ya kupikia. Hii ni hatua kubwa sana katika kuendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia. 

Na leo tunaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kugawa bila gharama yoyote mitungi hii ya Kilogramu 15 na majiko ya sahani mbili kwa watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Mara. Mkawe mabalozi wazuri wa nishati safi ya kupikia,” amesema Mjumbe huyo wa Bodi.

Awali, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mara, ACP. Hospitius Mendi amesema kuwa tangu kuanza kutumia nishati safi ya kupikia, Magereza wameokoa muda waliokuwa wanatumia kutafuta kuni pamoja na gharama za kusafirisha kuni.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya ametoa rai kwa watumishi wa jeshi la magereza wote nchini kutunza miundombinu ya nishati safi ya kupikia iliyofungwa katika magereza pamoja na kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia.