Wakazi wa vijiji 20 vilivyoko ukanda wa Ziwa Natron katika Wilaya ya Longido, mkoani Arusha, wamebadili maisha yao kiuchumi, baada ya Mradi wa Ardhi kwa Maisha, uliokuwa ukitekelezwa na Shirika la World Wide Fund for Nature (WWF), kutoa mchango wa haraka wa kipato na kuboresha maisha ya jamii za kifugaji, kupitia sekta ya mazingira na uchumi.
Mradi huo, ulikuwa ukilenga zaidi kuinua hali za maisha za wakazi wa maeneo yanayotishiwa na ukame na mabadiliko ya tabianchi, kwa kuwapatia ujuzi, fursa za kiuchumi na maarifa ya kulinda mazingira.
Wakizungumza jana, Wilayani hapa kwa nyakati tofauti, wakati wa ufungaji wa mradi huo, baadhi ya wanufaika akiwemo, Paulina Kelembwe na Losinyati Laizer, wameeleza kuwa mradi huo umeimarisha maisha ya wanawake kwa namna ya kipekee, kwa kuwapatia uelewa wa kifedha na fursa za kujitegemea, kupitia shughuli za ufugaji kuku na uanzishaji wa benki za wananchi vijijini (VIKOBA).
“Katika jamii yetu ya zamani, mwanamke hakuwa na nafasi ya kuuza au kumiliki mali, lakini kupitia mradi huu, sasa wanawake wanapata kipato, wanahudumia familia na kutoa mahitaji kwa watoto. Haya ni mabadiliko makubwa katika jamii yetu,” amesema Losinyati.
Mradi huo wa miaka miwili wa ‘Land 4 Life’ ulikuwa ukitekelezwa na WWF kwa kushirikiana na Shirika la Tanzania People & Wildlife (TPW).
Kabla ya kufungwa kwa mradi huo, Prof. Noah Sitati, ambaye ni msimamizi wa mradi huo, amezitaja shughuli mbalimbali zilizofanikishwa kupitia mradi huo, ikiwamo ufugaji wa nyuki na ugawaji wa mizinga, ufugaji wa kuku kwa mashine za kutotolesha, kilimo cha alizeti, mbinu za kudhibiti wanyama waharibifu, kuanzisha vikundi vya vikoba, mradi wa malisho na mbuzi wa kunenepesha.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Grace Mgase, amesema kuwa mradi huo umeleta manufaa makubwa kwa wananchi, kwa kuwa, mbali na kuongeza kipato na ujuzi, pia umeongeza ushiriki wa jamii katika shughuli mbadala za kiuchumi, tofauti na ufugaji pekee.
“Wananchi sasa wameanza kuachana na shughuli hatarishi kwa mazingira kama uwindaji haramu na ukataji wa miti, na badala yake wanashiriki katika uhifadhi wa mazingira, hali ambayo pia imeboresha lishe na ustawi wa familia,”ameongeza Mgase.
Alisema Halmashauri ya Wilaya hiyo, imeweka mikakati ya kuendeleza miradi hiyo, kwa kuimarisha umoja wa wazalishaji vijijini, kutoa mafunzo kupitia walimu wa kijiji, na pia kuhakikisha wanapata mikopo ya asilimia 10 kutoka kwenye mapato ya Halmashauri, kwa ajili ya kuboresha miradi iliyoanzishwa.
Akifunga rasmi mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salum Kalli, aliwashukuru wadau hao wa maendeleo waliotekeleza mradi huo, huku akiwataka kuendelea kushirikiana na serikali kwa kuleta miradi mingine zaidi.
“Longido kwa sasa ina amani na utulivu. Tunahitaji maendeleo. Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau wote wenye nia ya kuandika maandiko zaidi ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wetu,” amesema Kalli.
Mradi wa Ardhi kwa Maisha, unatajwa kuwa mfano wa kuigwa katika kusaidia jamii ya wafugaji, kuibua shughuli mbadala za kiuchumi zinazochangia katika uhifadhi wa mazingira na kuboresha maisha ya wananchi wa vijiji vya pembezoni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED