Wakati Klabu ya Azam FC, ikiibomoa Al Hilal ya Sudan kwa kumchukua Kocha Mkuu, Florent Ibenge, anayetarajiwa kutimka na wachezaji wapatao wanne, Klabu ya Simba nayo imeingia kwenye harakati ya kukibomoa kikosi hicho, ikihitaji saini ya beki wa kushoto, Khadim Diaw, raia wa Senegal.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo, pamoja na vyanzo vingine zinasema kuwa Simba imeingilia dili la JS Kabylie ya Algeria, ambayo ilikuwa ya kwanza kuonesha nia ya kumhitaji mchezaji huyo.
Viongozi wa Simba wameingia kwenye kinyang'anyiro cha kumhitaji beki huyo ili kumsaidia Mohamed Hussein 'Tshabalala' ambaye ameonekana anacheza michezo mingi kiasi cha kuchoka na kusababisha kutokuwa kwenye kiwango kizuri katika baadhi ya mechi.
"Diaw anatafuta changamoto mpya na tayari ameiambia Al Hilal kuwa hatokuwapo kwenye kikosi msimu ujao, rais wa klabu amemruhusu kuondoka.
"JS Kabylie waliwasiliana na wakala wake, lakini hawajatuma ofa rasmi. Simba wameingia kwenye mbio za kutaka kumsajili mchezaji huyo," chanzo kilisema.
Beki huyo alionekana kufanya vizuri kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akiichezea Al Hilal ya Sudan, iliyoishia kwenye hatua ya robo fainali.
Ilitolewa katika hatua hiyo na Al Ahly ya Misri, ilichapwa jumla ya mabao 5-0, bao 1-0 likifungwa Mauritania, kabla ya kuchapwa 4-0 ugenini nchini Misri.
Simba inayoonekana kuwa imedhamiria msimu ujao kuimarisha eneo la ulinzi, pia imeanza mazungumzo na Lusajo Mwaikenda wa Azam FC, kwenda kusaidiana na Shomari Kapombe, upande wa beki wa kulia, ambaye licha ya umri kwenda, lakini amekuwa akitumika kwenye michezo mingi.
Wakati hayo yakiendelea, klabu hiyo imempa mkataba wa miaka mitatu Morice Abraham, aliyekuwa akifanya mazoezi na timu hiyo kwa muda mrefu.
Habari zinasema kuwa, Kocha Mkuu, Fadlu Davids, ameonekana kuridhishwa na uwezo wake binafsi, ikiwa ni pamoja na kucheza nafasi nyingi uwanjani, kama winga ya kulia, kushoto, namba 10 na namba nane.
Mchezaji huyo alikuwa nahodha wa Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20, lakini kwa sasa umri wake umekuwa mkubwa zaidi ya hapo.
Viongozi wa Simba wameonekana kubadilika kwani awali walitaka kusajili wachezaji wachache kuelekea msimu ujao, lakini sasa wanataka ufanyike usajili wa nguvu kwani baadhi ya wachezaji ambao walikuwa wanawategemea kuwa wataibeba timu wameiangusha, huku viwango vyao vikionekana kushuka siku hadi siku.
Mfadhili wa zamani wa timu hiyo, Azim Dewji, amekiri kuwa kuna sehemu wamekosea kwenye usajili msimu uliopita, akisema baadhi ya wachezaji hasa wa kigeni hawakuwa na msaada, hivyo wataangalia jinsi gani ya kusajili wachezaji wazuri zaidi kuelekea msimu ujao.
"Tutasajili, tutasajili wachezaji bora kulingana na matakwa ya timu, moja ya vitu vilivyotuangusha ni usajili, baadhi hawakukidhi matakwa ya timu, wengine walikuwa bora, lakini viwango vyao vilikuwa vinashuka kila mchezo," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED