189 wachukua fomu ubunge Mororgoro, yumo Dokii

By Christina Haule , Nipashe
Published at 04:59 PM Jul 02 2025
Bendera za CCM
Picha: Mtandao
Bendera za CCM

WANACHAMA 189 wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge katika majimbo 11 mkoani Morogoro, kuanzia Juni 28 hadi Julai Mosi, mwaka huu.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, Nuru Ngereja, akitoa taarifa fupi ya wagombe waliochukua fomu, amesema matarajio kwa mkoa wa Morogoro wanaweza kufikia wanachama zaidi ya 200.

Anasema watajitokeza kuomba nafasi ya kuteuliwa kugombea uwakilishi wa majimbo ya uchaguzi kwa nafasi hizo.

Aidha Katibu Ngereja alisema jumla ya wanachama 14 wameonesha nia ya kugombea kwa kutia nia na kuchukua fomu na kurejesha katika Jimbo la Morogoro Mjini hadi leo.

Akizungumzia ubunge Viti Maalum, kupitia Umoja wa wanawake kwa mkoa wa Morogoro wenye nafasi za uwakilishi kupitia mkoa, Taasisi zisizo za kiserikali (NGOs), kundi la Walemavu na kundi la vyuo vikuu anasema wanachama 31 walioonesha nia ya kuomba dhamama ya chama kugombea nafasi hizo kupitia ubunge viti maalum.

Ngereja anasema katika ngazi ya kata kwa nafasi za udiwani pia wagombea wamejitokeza kwa wingi wakiwemo wanaume, vijana, kinamama na hata wenye ulemavu.

Mmoja wa wagombea viti hivyo, mkoa wa Morogoro ambaye ni msanii wa tasnia ya uigizaji Ummy Wenslaus, kwa jina maarufu Dokii, amesema amelazimika kuchukua fomu na kurejesha kugombea ubunge, ili kutatua changamoto za wanawake ikiwemo ukosefu wa ajira na mitaji sambamba na kusaidia vizazi vya kinamama hao katika kusimamia maendelelo ya Watoto wao.

Mgombea mwingine Pudensiana Munishi, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Morogoro, amesema amelazimika kuchukua fomu na kurejesha, ili kuwatumikia wana Morogoro katika masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo changamoto za wanawake, watoto na hata wenye ulemavu.

Uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea nafasi za ubunge na udiwani katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu, zimeanza kutolewa Juni 28 na kutakiwa kumalizika Julai 2, mwaka huu.