Nderiananga adai miili 2 bado DNA haijakubali

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 11:15 AM Jul 03 2025
Miili ya waliofariki kwenye ajali ya Same
Photo: Mpigapicha Wetu
Miili ya waliofariki kwenye ajali ya Same

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga, amesema bado Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS), inaendelea kuchunguza miili ya watu wawili waliofariki katika ajali ya barabarani iliyotokea Wilaya ya Same, na kuchukua maisha ya watu 42.

Kwa mujibu wa Nderiananga, miili hiyo haijatambuliwa katika uchunguzi wa sampuli za vipimo vya vinasaba (DNA), na sasa MMS inaendelea na kazi mpaka i-match (vioane na sampuli za vinasaba vya ndugu zake) na ikakamilika watakabidhiwa kwa familia husika.

Ajali hiyo iliyotokea Juni 28 mwaka katika la Sabasaba, Kitongoji Mahuu, Kata ya Same, takribani kilomita nne kutoka Same mjini, ililihusisha basi kubwa la abiria, Mali ya Kampuni ya Chanel One, lenye namba za usajili T 179 CWL na basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster, lenye namba T 199 EFX linalomilikiwa na Kampuni ya Mwami Trans.

Coaster hiyo, ilikuwa ikitokea Same kuelekea Manispaa ya Moshi, wakati basi la Chanel One lilikuwa likitokea Arusha kuelekea Tanga.