Samia ataka haki vikao vya uchujaji majina wagombea

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 04:43 PM Jul 03 2025
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla.

Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, amevielekeza vikao vya uchujaji wa majina watakaopeperusha bendera nafasi ya ubunge, uwakilishi na udiwani, vikatende haki na si majungu na fitina.

Kauli hiyo imetolewa baada ya kukamilisha mchakato wa awali wa uchukuaji fomu, ambapo walioomba ridhaa nafasi ya ubunge kupitia majimbo Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar ni wanachama 4,109, ambapo kati yao 3,585 kutoka Bara na 524 Visiwani Zanzibar.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, aliyasema hayo leo Julai 3,2025, wakati akitoa taarifa ya mchakato wa CCM wa uchukuaji fomu uliofanyika kwa siku tano kuanzia Juni 28, mwaka huu, na kuhitimishwa jana.

“Ni maelekezo kwa niaba ya Halmashauri Kuu ya Taifa kupitia Mwenyekiti wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan, anaelekeza vikao vyote vitakavyofanya uchujaji na uteuzi, viwatendee haki wagombea, visionee watu.

“Vitende haki na haki ionekane ikitendeka, tusitengeneze fitina na majungu katika mchakato huu wa uteuzi. Tutende haki na kuteua watu kwa haki na tusimwonee mtu,” amesema.

Makalla amesema wanapokwenda katika uchaguzi chama kitakuwa na mambo ya kusema, mafanikio yaliyofanywa na serikali na Ilani, na yote yatanogeshwa kwa kuwa na wagombea wazuri.

“Chama Cha Mapinduzi kimefurahishwa na hamasa kubwa iliyojitokeza katika mchakato huu. Ninyi ni mashahidi uchukuaji wa fomu CCM safari hii umevunja rekodi, habari ya mjini ni uchukuaji fomu CCM.

“Hii inaonesha CCM kinaaminika kwa Watanzania na ni chama imara, kina sera nzuri na ndio matumaini ya Watanzania. Tumeona makundi mbalimbali yamechukua fomu, vijana, wanawake, watu wa kila rika wamechukua fomu,” amesema Makalla.