Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewaelekeza wakuu wa wilaya kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati ili kusaidia kuendeleza amani na utulivu katika maeneo yao ya kazi Kanali Mtambi ametoa maelekezo hayo mjini Musoma leo, wakati akiwaapisha wakuu wa wilaya wawili wapya walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kupelekwa katika wilaya za Butiama na Serengeti.
Wakuu wa wilaya hao ni Angelina Lubela wa Butiama na Thecla Mkuchika wa Serengeti ambao waliapishwa kabla ya kwenda kwenye vituo vyao vya kazi walivyopangiwa.
"Malalamiko, kero na migogoro ya wananchi ikitatuliwa kwa wakati itasaidia kuleta amani na utulivu katika jamii na kuwarahisishia kufanya shughuli zao za maendeleo," amesema Kanali Mtambi.
Aidha, amewaelekeza kusimamia mchakato wa uchaguzi katika maeneo yao ili ufanyike kwa uwazi kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kuwaonya watakaouharibu hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Mbali na hilo, amewataka kusimamia suala la utoaji wa chakula shuleni na kuwahamasisha wazazi, walezi, wadau wa elimu kuchangia chakula ili wanafunzi wapate angalau mlo mmoja kwa siku.
"Pia mzisimamie halmashauri katika ukusanyaji wa mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuimarisha makusayo ya halmashauri na kuzifanya ziwe imara kiuchumi kuwahudumia wananchi," amesema.
Amewaagiza pia kufuilia na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao na kuzigeuza changamoto mbalimbali watakazokutana nazo kuwa fursa za kimaendeleo.
"Mmeaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, nindeni mkasimamie utekelezaji wa shughuli za serikali katika wilaya zenu kwa manufaa ya wananchi wa wilaya hizo na mkoa kwa ujumla," amesema.
Akizungumza kwa niaba yao, mkuu wa wilaya ya Musoma, Juma Chikoka ameahidi kuwapa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao wakuu hao wa wilaya wapya.
"Mkoa wa Mara tunaishi kwa mshikamano na kushirikiana kama familia moja, katika kuwahudumia na kutatua kero za wananchi na kutekeleza maagizo ya viongozi wetu” amesema Chikoka.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED